Sunday 8 December 2013

Baba Asusia Mazishi ya Mwanae Ambae alikuwa Jambazi..

Mkazi wa kijiji cha Karoto geita, Isaya Ngarama, amekataa kumzika mtoto wake, Samwel Isaya (27), ambaye aliuawa na wanakijiji kwa tuhuma za ujambazi na mwili wake kuteketezwa kwa moto.
Samwel, aliuawa akiwa na mwenzake na miili yao kuchomwa moto juzi baada ya wanakijiji kuwahusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu.

 
 Tukio hilo lilitokea juzi jioni baada ya Jeshi la Polisi mkoani Geita, kutoa idhini ya kuzikwa kwa miili ya watu hao waliouwa kikatili kwa kipigo kikali kutoka kwa wananchi.
Baada ya mzazi huyo kukataa kumzika mtoto wake, wanakijiji waliamua kuuzika wa mtuhumiwa mwingine ambaye hakufahamika jina na mahali alikotoka huku wakiuacha mwili wa Samwel uliotambuliwa, uandaliwe taratibu za mazishi na wanafamilia.

Hata hivyo, katika hali isiyotarajiwa, baba wa marehemu huyo alikataa kata kata kuuzika mwili huo kwa madai kuwa alichukizwa na tabia ya mwanawe ya uhalifu.

Hatua hiyo iliufanya uongozi wa serikali ya kijiji hicho ukiongozwa na Mwenyekiti, Joel Mazemule na Ofisa Mtendaji wake, Peter Chota, kuukubali  mwili huo uzikwe kiserikali.

Baba wa marehemu huyo alifafanua kuwa mtoto wake wakati wa uhai, alikuwa akijihusisha na udokozi na alimkemea mara kadhaa lakini hakubadilika.

Hata hivyo, uongozi wa kijiji hicho kwa kuwashirikisha  baadhi ya wazee wa kijijini hapo, walimshauri Isaya na akakubali kushiriki mazishi ya mtoto wake kama wanakijiji wengine.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Prudenciana Protas, juzi alithibitisha kuuawa  kwa watu hao wawili wakituhumiwa majambazi na miili yao kuchomwa moto.

No comments: