Monday 9 December 2013

CHADEMA yadinda

Katibu Mkuu, Dk. Slaa JITIHADA za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutumia mzozo kati ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) zinaelekea kugonga mwamba.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa CCM imewekeza vya kutosha katika hujuma dhidi ya CHADEMA ikitumia baadhi ya wanachama wa zamani wa chama hicho kuunda mgogoro na kukipasua.


Hata hivyo, licha ya misukosuko na kelele kutoka kwa baadhi ya wanachama na wanaodhaniwa kuwa ‘mapandikizi’, CHADEMA kimeweza kupuuza hujuma hizo na kujikita katika harakati za ujenzi wa ngazi za chini za chama katika vijiji na vitongoji.
Kwa sasa viongozi kadhaa wa CHADEMA wamesambaa katika majimbo 103 nchi nzima kujenga chama kwa kufuata maagizo ya Baraza Kuu lililoketi mwishoni mwa mwaka jana, kama mwendelezo wa vuguvugu la mabadiliko, na ujenzi wa chama kuelekea uchaguzi unaokuja.
Baadhi ya wanachama walioondolewa kwa tuhuma mbalimbali wamekuwa wanashirikiana na wana CCM waziwazi kusambaza maneno machafu dhidi ya CHADEMA mtandaoni na mitaani. Baadhi yao wameshiriki kutengeneza mabango na kuyapeperusha katika mikutano inayohutubiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, katika mikoa ya Shinyanga na Kigoma.
Wanapinga uamuzi wa Kamati Kuu kuwavua nyadhifa Zitto, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba. Zitto amevuliwa wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu, Dk. Kitila amevuliwa wadhifa wa Mjumbe wa Kamati Kuu, na Mwigamba amevuliwa wadhifa wa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za ‘usaliti’.
Katika kumtetea Zitto na wenzake, baadhi ya wanachama wamekuwa wakitoa matamko, huku wawili wakitangaza kujiuzulu nafasi zao katika mikoa ya Lindi na Singida.



No comments: