Sunday 8 December 2013

Dk. Slaa akemea ukaburu wa CCM


Dk. Willibrod SlaaKATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema wakati Rais Jakaya Kikwete ametangaza siku tatu za maombolezo kwa kifo cha Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, serikali yake inapaswa kumuenzi kwa kuacha kufanya vitendo vya ‘kikaburu’ kwa raia wake.
Dk. Slaa amedai kuwa baadhi ya mambo ya kikatili wanayofanyiwa wananchi wa Tanzania na serikali yao, hususan kupitia vyombo vya dola, yameanza kufanana au hata kuvuka viwango vya ukatili walivyofanya makaburu wa Afrika Kusini dhidi ya Mandela na wenzake wakati walipokuwa wakipiga vita ubaguzi wa rangi na utawala wa weupe wachache nchini humo.
Kiongozi huyo aliyasema hayo jana katika mikutano yake ya hadhara katika Kijiji cha Mabamba na mjini Kibondo, mkoani Kigoma akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya ujenzi na kukagua uhai wa chama hicho katika mikoa ya Shinyanga, Kigoma, Tabora na Singida.
“Wananchi, Watanzania wenzangu, msiba wa Mzee Mandela kwetu sisi Tanzania ni msiba mzito na mkubwa. Wakati wenzetu kwa maana ya Afrika na dunia kwa ujumla wakiomboleza, pia sisi kwetu ni msiba wa ndugu na jamaa wa karibu. Mtakumbuka kuwa tuliwapatia hifadhi wakimbizi na wapigania uhuru kutoka Afrika Kusini.
“Walipokaa kwetu hapa, katika maeneo mbalimbali ya nchi, wengine waliwahi kuacha watoto na wajukuu nchini kwetu…hivyo mahusiano yetu yalivuka mipaka ya nchi na nchi. Mtakumbuka wakati fulani jeshini, JKT, shuleni kwenye mchakamchaka na kila mahali tulikuwa tunaimba ‘kaburu chinja’.
“Wakati tunaimba ‘kaburu chinja’, akina Mandela nao walikuwa mstari wa mbele kupambana kumwondoa kaburu huyo. Ilifikia hatua Mandela aliitwa ni gaidi kwa sababu ya kupigania haki na matumaini ya wananchi wake weusi wengi wa Afrika Kusini. Wakaamua kumfunga maisha jela, akakaa miaka 27 gerezani.
“Ninachotaka kusema ni kwamba, Mandela alikuwa mpigania haki, alipiga unyanyasaji wa dola dhidi ya raia, alipinga dhuluma ya watawala kwa watu walio chini, leo hii serikali hii ya CCM inafanya hayo hayo ambayo waliyafanya makaburu, na Mandela akapambana kuhakikisha yanaondoka na leo dunia nzima inaimba ushujaa wake wa ukweli. Hakuwahi kusaliti wananchi wake katika kupigania haki na utu wa mwanadamu, alikuwa tayari kufa,” alisema Dk. Slaa na kuongeza;
“Yanayofanyika leo wananchi wangu ni hatari kuliko ya makaburu. Sisi tunao ushahidi wa wazi wa namna vijana wetu waliotuhumiwa kesi ya ugaidi walivyofanyiwa vitendo vya kinyama kwa kuingiziwa midenge sehemu za siri na chupa, wakapigwa shoti za umeme ili waseme kuwa Dk. Slaa au Mbowe waliwatuma.”
Akiendelea kutaja mifano mbalimbali ya vitendo vya kikatili alivyodai kuwa vinafanywa na serikali dhidi ya raia wake wasiokuwa na hatia, Dk. Slaa alimtaka Rais Kikwete atafakari kuhakikisha anachukua hatua za kuachana na vitendo ambavyo Watanzania waliwahi kuimba usiku na mchana kuvipinga, wakiwaunga mkono wapigania uhuru wa Afrika Kusini.
Ashangaa CCM kuionea huruma CHADEMA
Akihutubia mkutano wa Mabamba mapema asubuhi jana, Dk. Slaa alisema kuwa anashangazwa na hatua ya wana CCM kuonekana kuumizwa au kulalamika, kila inapotokea CHADEMA imechukua hatua ya kinidhamu ndani ya chama hicho kutokana na tuhuma za ama viongozi au wanachama.
Alisema hayo baada ya jana pia kama ilivyokuwa juzi Kakonko, walijitokeza vijana wapatao saba wenye mabango yaliyoonekana kutuma ujumbe kwa viongozi na chama hicho kupinga maamuzi ya vikao vya Kamati Kuu vilivyomvua nafasi ya uongozi Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na wenzake wawili, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba.
Katika mazingira yale yale yanayofanana na juzi mjini Kakonko, huku baadhi ya wahusika wakiwa ni wale wale, mara baada ya msafara wa Dk. Slaa kuwasili eneo la mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mpira wa Mabamba, kulitokea kikundi cha vijana wapatao saba na mabango yao, ambapo polisi waliokuwepo walitaka kuwaondoa kwa nguvu, kabla kiongozi huyo hajaingilia kati kuwazuia.
Kama ilivyokuwa kwa Kakonko, mabango ya vijana hao yalikuwa yameandikwa kwa hati moja ya mwandiko yakiwa katika karatasi, ambapo gazeti hili liliweza kubaini mmoja wao alikuwepo katika mkutano wa Kakonko ambako alikiri mbele ya hadhara kuwa yeye ni mtoto wa mstaafu wa mwenezi wa CCM.
Akiwa amefanya hivyo hivyo mjini Kakonko, Dk. Slaa aliwataka vijana hao wachukue nafasi ya mbele kwenye mkutano wake ili aweze kuona ujumbe wao na aweze kuwajibu kama walihitaji ufafanuzi wa masuala ya kikatiba ya chama hicho, hususan yanayohusu walichokuwa wameandika katika mabango hayo.
Vijana wale walisogea mbele ambapo Dk. Slaa alishuka jukwaani kurudi mezani kwake akisubiri itifaki za kawaida, lakini badala ya kutulia, vijana wale wakaanza kupiga kelele, wakikataa kupigwa picha na waandishi wa habari wa magazeti na televisheni, hali ambayo iliondoa uvumilivu wa askari polisi.
Baada ya askari polisi kuanza kuonyesha nia ya kuchukua hatua ya kumaliza zogo lile kwa kuanza kuwasogelea vijana wale, Dk. Slaa alitoa ruksa ya kuondolewa akisema kuwa wameshindwa kuheshimu demokrasia aliyowapatia ya kutoa hisia zao, badala yake wanaonekana kuwa na lengo la kuvuruga mkutano huo wa kisheria.
“Jamani Watanzania wenzangu nimeambiwa hawa vijana wanajulikana hapa. Ni vijana wa CCM wala si vijana wa CHADEMA na wanaonekana kuwa wamelewa, hata ninyi hapa mnasema hivyo. Sasa kama mtu una wazo lako na unafikiri ni zuri kwanini unasubiri kwanza kupewa pombe ndiyo uje hapa useme.
“Mwana CHADEMA anayeheshimu chama chake hawezi kufanya hivyo. Sasa kinachonishangaza ambacho itabidi tujue maana yake ni nini, eti wana CCM wanaonekana kuipenda CHADEMA na kumhurumia zaidi Zitto, hivi kuna mtu wa CCM anaweza kumpenda Zitto kuliko wana CHADEMA wenyewe?” alihoji Dk. Slaa.
Dk. Slaa alisisitiza kusema kuwa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu waliahidi Watanzania kuwa iwapo wangewapatia dhamana ya kuongoza nchi, chama chake kingeenda kusimamia na kurudisha hali inayoonekana kuparaganyika ndani ya nchi katika mstari sahihi, akiongeza kuwa hatua kama hizo za kusimamia serikali zinaweza kuchukuliwa ndani ya chama.
Aliongeza kuwa iwapo chama hicho kitashindwa kuchukua hatua na kukisaidia kujisahihisha, kisha kikaanza kupindisha hata misingi yake, ikiwemo kusimamia katiba yake, hakitaweza kufaa kukabidhiwa mamlaka na dhamana ya kuongoza dola.
Wakati huo huo, viongozi wa CHADEMA wameanza kufuatilia nyendo za kijana mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Salum, wakidai kuwa amesafiri kutoka Kigoma mjini, akipitia Kibondo, kisha Kakonko, akifanya kazi ya kutafuta vijana wa CCM au wahuni wa mitaani kisha anawapatia fedha na kuwanywesha pombe ili wabebe mabango kwenye mikutano ya chama hicho.
Habari ambazo gazeti hili limezipata kutoka vyanzo vyake ndani ya chama hicho, zimesema kuwa mtu huyo amekuwa akipita siku moja kabla, kila mahali ambapo Dk. Slaa anatakiwa kwenda kufanya mikutano, ambapo maeneo ya Kakonko alijaribu kuwarubuni viongozi wa chama hicho wafanye mbinu za kuhujumu lakini wakamkatalia.
Wakati huo huo,  Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, anatarajiwa kuanza ziara jijini Mwanza, ambako pamoja na mambo mengine atahutubia mikutano ya hadhara.
Mbowe anatarajiwa kuwasili jijini Mwanza Desemba 14, ambapo atafanya kazi za kujenga na kuimarisha chama, ikiwa ni pamoja na kuzindua Mkoa wa Vyuo Vikuu.
Hayo yamethibitishwa jana jijini Mwanza na uongozi wa CHADEMA tawi la Chuo Kikuu cha St Augustine (SAUT), walipokuwa wakijibu maswali ya waandishi wa habari, katika kikao cha wasomi hao cha kutoa tamko la kuunga mkono uamuzi uliofanywa na Kamati Kuu ya chama hicho kuwavua uongozi Zitto Kabwe, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba.

No comments: