Monday 9 December 2013

Mbunge: Wajumbe mabaraza ya ardhi wapigwe msasa

                      MBUNGE wa Biharamulo, Dk. Anthony Mbassa (CHADEMA), ameitaka serikali ieleze ina  mikakati gani ya kuwasaidia wajumbe wa mabaraza ya ardhi ambao hawana uelewa wa kisheria.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo bungeni jana alipokuwa akiuliza swali na nyongeza na kuhoji kwa nini serikali isiwatumie wanasheria wa halmashauri kuwawezesha kielimu wajumbe hao.
Pia aliitaka serikali kuangalia uwezekano wa kuyajengea uwezo mabaraza hayo, ili kufanya shughuli zao kwa kiwango kizuri ambacho kitaondoa malalamiko.
Katika swali la msingi, mbunge wa Viti Maalum, Sara Msafiri (CCM), alitaka kujua ni lini serikali itabadilisha mfumo wa mabaraza hayo na kuupeleka katika mfumo wa mahakama.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, alisema serikali haina nia ya kuvunja mabaraza ya ardhi yaliyopo na kuyaunganisha  na mfumo wa mahakama.
Kombani alisema nia ya kutovunja mabaraza hayo ni kutokana na ukweli kuwa kwa kufanya hivyo ni kurudisha mlundikano wa kesi ndogondogo mahakamani.
Alisema mabaraza ya ardhi ya vijiji yaliundwa kwa lengo la kusuluhisha migogoro ya ardhi iliyoletwa mbele yake, ili kuleta mapatano kati ya wahusika  kwa njia ya usuluhishi.
Alisema kutokana na hali hiyo mabaraza hayo hayaongozwi wala kufungamana na taratibu za mfumo wa mahakama bali huzingatia misingi ya haki za asili  ili haki itendeke na ionekane imetendeka.

No comments: