Tuesday 10 December 2013

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Ashton atarajiwa Ukraine

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Cathrine Ashton yuko Ukraine katika juhudi za kuutatua mgogoro wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo. Ashton anatarajiwa kukutana na Rais Viktor Yanukovych baadae leo
Polisi wakipambana na wapinzani wa serikali Polisi wakipambana na wapinzani wa serikali
Mkuu huyo wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Cathrine Ashton anawasili nchini Ukraine wakati mvutano umezidi kuwa mkubwa baina ya polisi na wapinzani wa serikali. Leo asubuhi polisi walipambana tena na waandamanaji katika mji mkuu wa Ukraine Kiev.
Mbunge wa chama cha Uhuru ameliambia shirika la habari la AFP kwamba watu zaidi ya 10 walijeruhiwa katika mapambano hayo.Waandamanaji kadhaa wamevunjika miguu au mikono. Na idara za serikali zimearifu kwamba polisi wawili pia walijeruhiwa.
Hapo jana polisi walizibomoa kambi za waandamanaji zilizokuwapo nje ya majengo ya serikali. Kwa muda wa wiki kadhaa wapinzani walikuwa wametanda katika mji wa Kiev wakiandamana kupinga uamuzi wa Rais Viktor Yanukovych wa kukataa kuutia saini mkataba wa biashara huru na Umoja wa Ulaya na kuishirikisha Ukraine katika Umoja huo. Wapinzani wa serikali wanataka nchi yao ijiunge na Umoja wa Ulaya. Lakini polisi waliotanda katika mji wa Kiev waliandelea hadi usiku wa jana kuwakabili waandamanaji.
Kiongozi wa upinzani, bingwa wa masumbiwi za uzito wa juu Vitali Klitschko amesisitiza kwamba lazima Ukraine iwe sehemu ya Ulaya.Amesema kwa muda wa miaka zaidi ya 20 watu wa Ukraine wamekuwa wanaishi na matumaini ya kuwa na nchi ya kisasa na ya kidemokrasia.
Wakati huo huo Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Bibi Ashton anaewasili leo nchini Ukraine anatarajiwa kukutana na Rais Viktor Yanukovych katika juhudi za ,kuutatua mgogoro wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo.Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari naibu Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Victoria Nuland pia anatarajiwa kuwasili nchini Ukraine leo.Mbali na kukutana na Rais Yanukovych Ashton na Nuland pia watakutana na viongozi wa upinzani.
Rais Yanukovych pia atakutana na marais watatu wa hapo awali ikiwa pamoja na Viktor Yushchenko aliemshinda Yanukovych katika uchaguzi wa mwaka 2004 uliofanyika kutokana na shinikizo la waandamanaji.
Maandamano ya kuupinga uamuzi wa Rais Yanukovych wa kukataa kuutia saini mkataba na Umoja wa Ulaya sasa yanaingia katika wiki ya tatu nchini Ukraine.Rais Yanukovych alifikia uamuzi huo kutokana na shinikizo kubwa la Urusi.

No comments: