Saturday 7 December 2013

NATAKA KWENDA ULAYA "SAMATA"


 
 MCHEZAJI WA TP MAZEMBE NA TIMU YA TAIFA YA TANZANIA MBWANA SAMATA


Mshambuliaji tegemeo wa timu ya soka ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), Mbwana Samatta, amesema hana muda mrefu kabla ya kwenda kucheza soka Ulaya baada ya klabu mbalimbali za barani humo kuhitaji huduma yake kwa sasa.

Samatta ambaye anaichezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, alitua jijini Nairobi Desemba 2, mwaka huu na kuungana na Kikosi cha Bara na kuifungia bao pekee juzi ilipocheza na Burundi katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi.

Akizungumza na NIPASHE jijini hapa juzi, Samatta, alisema ni mapema kuzitaja klabu hizo zinazomhitaji, lakini ana hakika kwamba kwa sasa yuko njiani kujiunga na klabu ya nje ya Bara la Afrika.

"Ningekutajia klabu na nchi inayonihitaji, lakini ukweli Dada yangu, mimi bado nina mkataba na TP Mazembe na huwa haituruhusu kuongea na vyombo vya habari masuala ya mikataba yetu. Nikifanya hivyo nitachukuliwa hatua ila kweli ninatakiwa na klabu kubwa nje ya Afrika," alisema Samatta.

Akikizungumzia Kikosi cha Kili Stars, Samatta ambaye alisajiliwa na TP Mazembe akitokea Simba, alisema anaamini kinaweza kufanya vizuri msimu huu tofauti na mwaka jana ambapo ilifungwa kwenye mechi ya kuwania mshindi wa tatu na Zanzibar (Zanzibar Heroes).

Aliongeza kuwa, ushindani ulioko katika kila mechi wanazocheza ndiyo unawaimarisha na ujio wake na mshambuliaji mwenzake, Thomas Ulimwengu, umeongeza nguvu katika timu ya Kilimanjaro Stars.

"Kila hatua tunayosonga ndiyo timu inazidi kujiimarisha, haturudi nyuma kamwe, ninaamini tutafanya vizuri pia siku ya Jumamosi," aliongeza mshambuliaji huyo wa zamani wa African Lyon ya jijini Dar es Salaam.

Kdhalika Samatta alieleza kuwa anafurahia kuona kikosi cha mwaka huu kinaundwa na wachezaji wengi chipukizi ambao watakuwa na muda mrefu wa kuichezea timu hiyo katika mechi mbalimbali za mashindano zitakazofanyika mwakani.

Aliwataka pia mashabiki wa soka wa nyumbani kutoa ushirikiano kwa wachezaji wao na kuwaamini wanapoteuliwa.

Kilimanjaro Stars iliyoko chini ya Kocha Mkuu, Mdenmark Kim Poulsen, ilimaliza Kundi B ikiwa na pointi saba sawa na vinara Zambia ambao wana wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, Burundi ikifuatia na Somalia iliyotolewa kwa kufungwa mechi zake zote tatu.

No comments: