Monday 16 December 2013

SIMBA YA ZUBAA KWA OKWI YANGA YA MNYAKUA KAMA MWEWE

USAJILI wa kishindo, Yanga imefanya kufuru kwa kufunga dirisha dogo la usajili kwa kumsajili kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Arnold Okwi na ataanza kuichezea klabu hiyo kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.
Okwi, ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya Uganda, The Cranes, amesaini kuichezea Yanga kwa miaka miwili na nusu na Shirikisho la Soka la Uganda (Fufa) limemuidhinisha rasmi kuwa mchezaji wa Jangwani.

Emmanuel Okwi akiweka alama ya dole gumba mbele ya Mjumbe wa Kamati ya Mashindano wa Yanga, Musa Katabaro (kushoto) wakati akisaini mkataba wa kuichezea Yanga miaka miwili na nusu mpaka mwishoni mwa msimu wa 2015/2016. Kulia ni Mwanasheria/Meneja wa Okwi, Edgar Agaba.

Mjumbe wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdallah Bin Kleb, amelithibitisha hilo kwa Championi Jumatatu na taarifa zinasema Okwi atatua nchini keshokutwa.

“Kweli tumemsainisha Okwi kwa muda huo na kila kitu kiko safi, tumefuata taratibu zote kupitia mtandao wa Fifa wa uhamisho na tumepata ITC, hivyo Okwi ni mchezaji halali wa Yanga,” alisema Bin Kleb.
Taarifa zinaeleza Yanga imemwaga zaidi ya Sh milioni 180 ili kumpata Okwi ambaye anajulikana kwa kasi, krosi safi na uwezo wa kufunga mabao katika wakati mgumu.

Awali, Simba ‘ilimuuza’ Etoile du Sahel (ESS) kwa kitita cha dola 300,000 (Sh milioni 480) lakini malipo yamekuwa hadithi na uongozi umekuwa mkali sana kuhusiana na hilo.

Baadaye akasusa kuichezea ESS kutokana na kutolipwa mshahara wake, baadaye akarejea SC Villa ya kwao Uganda ambako Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) likamuidhinisha acheze kwa mkopo.
Taarifa nyingine zinasema Okwi alisaini rasmi kuichezea Yanga Jumatano iliyopita na kila kitu kilifanyika jijini Kampala baada ya ‘jeshi’ la usajili la Yanga kuvamia mjini humo na kumaliza zoezi hilo.

Kila kitu kikafanywa siri kubwa kwa kuwa Yanga ilitaka kupata uhakika kwa kupokea ITC ambayo imepatikana jana ikiwa ni siku ya mwisho ya dirisha dogo la usajili.
Okwi alikuwa ‘roho’ ya ushambuliaji Simba, kipenzi cha mashabiki Msimbazi na tishio kwa Jangwani, lakini sasa huenda mambo hayo yakageukia upande wa pili.

No comments: