Wednesday 11 December 2013

Simba yafuta makosa ya Cannavaro, Yondani

KOSA la kumzuia straika Amisi Tambwe lililofanywa na mabeki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani hadi akapiga pasi kwa mfungaji Betram Mombeki, sasa linafanyiwa kazi na kikosi cha Simba.
Mombeki alifunga bao hilo dakika ya 54 baada ya kupokea pasi murua ya Tambwe ambaye aliwazidi ujanja Yondani na Cannavaro ambao walijipanga vibaya kwa kumzuia Tambwe lakini straika huyo aliwazidi ujanja na kumpa pasi mfungaji.
Katika pambano hilo la Ligi Kuu Bara lililochezwa Oktoba 20, mwaka huu kaika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Yanga ilikuwa ikiongoza kwa mabao 3-0 hadi mapumziko lakini Simba ilisawazisha mabao yote kipindi cha pili.
Kwa muda mrefu kwenye mazoezi ya Simba mwishoni mwa wiki iliyopita, Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic ameonekana akiwahimiza mabeki wake hasa wa kati kusimama katika nafasi sahihi wakati timu inaposhambuliwa.
Logarusic alionekana akitilia mkazo sehamu ya kusimama mabeki wake na mara kwa mara alikuwa akiwaelekeza kwa ukali baadhi ya mabeki waliokuwa wakirudia makosa ya kutokuwapo sehemu husika. Kocha huyo alienda mbali zaidi kwa kuwafundisha mabeki wake namna ya kusimama wanapokuwa wanakaba jambo lililokuwa likishangiliwa na mashabiki wachache wa Simba waliohudhuria mazoezi hayo.
Muda mfupi baada ya mazoezi hayo, Logarusic raia wa Croatia aliliambia Mwanaspoti; “Beki yeyote mzuri lazima awe anajua mahala sahihi pa kusimama na usimamaji wake unapaswa kuwa madhubuti ndiyo maana umeona nawasisitizia.”

No comments: