Monday 9 December 2013

Tambwe amsoma Logarusic kwa saa sita

STRAIKA wa Simba, Amissi Tambwe, amesema sasa anajua ujanja wa kocha mpya wa Simba, Mcroatia Zdravko Logarusic, baada ya kuangalia staili yake ya ufundishaji kwenye ‘You Tube’ kwa takribani saa sita.
Tambwe anasema aliziangalia video hizo kwa lengo la kujua ni vipi ataweza kuendana na staili ya ufundishaji wa kocha huyo na pia kujua atawezaje kupata nafasi ya kufunga mabao.
Mshambuliaji huyo ambaye yupo kwao Burundi mapumzikoni, alisema anatarajia kutua Tanzania wiki ijayo kwani anangoja viongozi wa klabu yake wamtumie tiketi.
“Nataka kuwa mfungaji bora na kuisaidia timu yangu kutwaa ubingwa, lakini ni lazima ujue kocha anataka nini, pia inabidi ucheze kuendana na staili anayoitaka. Hivyo mimi niliona ni bora nianze kumtizama mapema kabla hatujakutana,” alisema.
“Kwa mtazamo wangu baada ya kuangalia video zake akiwa na Gor Mahia ya Kenya na timu nyingine za Ghana, niligundua kuwa katika timu yake amekuwa akiwatumia washambuliaji ipasavyo, hivyo kwa staili hiyo bila shaka nitailetea Simba mafanikio.
“Huyo kocha mpya anaonekana anapenda mabao mengi na anataka straika asiwe na masihara anapokuwa karibu na lango. Lakini pia anataka viungo wanaopandisha mashambulizi, kocha atafurahia mambo yangu.”
Straika huyo aliongeza: “Itakuwa wakati wa Simba kurudi kileleni, falsafa na staili ya ufundishaji ya mwalimu itaturudisha juu kama timu.”
Naye Logarusic alisema: “Bado sijawajua mastraika wangu vizuri, wakianza mazoezi nina uhakika tutajua tusaidiana vipi na wapi watanifaa.
“Najua kuwa straika wa Simba (Tambwe) ndiye anayeongoza kwa magoli, nafikiri ni kitu kizuri cha kuanzia. Hivyo nitahakikisha anazidi kuisaidia timu akishirikiana na wenzake.”
Kwa upande wake, mshambuliaji, Betram Mwombeki, alisema: “Mimi nitahakikisha nakuwa kikazi zaidi, timu itakayokuja mbele yangu lazima ijue mimi nafanya kazi gani Simba. Sitaki kuongea sana kwani mikakati yangu ya sasa ni kufanya kazi.”





Tambwe akishangilia bao na wachezaji wenzake wa timu ya Simba 

No comments: