Monday 9 December 2013

Tanesco kufikishwa mahakaman

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), huenda likafikishwa mahakamani wiki hii na kudaiwa fidia ya mabilioni baada ya kusitisha mkataba wa kampuni ya kukarabati na kusafisha njia za umeme bila kuuzima. Kampuni hiyo ya MacDonald Live Line Technology, imeamua kuchukua hatua hiyo baada ya Tanesco kuishinda katika usuluhishi wa mgogoro wa kusitisha mkataba huo bila sababu za msingi.

Msuluhishi wa mgogoro huo, aliipa ushindi Tanesco na kuitaka MacDonald kulipa gharama kwa shirika hilo kama fidia na usumbufu uliotokana na kutokamilisha kazi iliyopewa katika Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Kampuni hiyo ilipeleka malalamiko yake kwa msuluhishi ambaye ni Wakili Mtango Jonathan Lukwalo, baada ya Tanesco kusitisha mkataba kwa kampuni hiyo kwa madai ilichelewa kutekeleza kazi ya ukarabati wa njia za umeme mkoani Arusha.

Tanesco na kampuni hiyo waliingia katika mkataba Machi, 2010 wa kufanya ukarabati wa njia ya umeme njia ya Kilimanjaro-Arusha kwa kutafuta nguzo na kuzisafirisha kwenda eneo la kazi.

Kazi hiyo ilitakiwa kukamilika ndani ya wiki 32 kuanzia Julai 28, 2010 hadi Machi 9, 2011.

Katika uamuzi wake wa mwezi uliopita, Wakili Lukwalo, aliiamuru kampuni hiyo kuilipa Tanesco Sh milioni 700 kwa kuchelewesha kazi na kuwasababishia hasara.

Kutokana na uamuzi huo, Mkurugenzi wa MacDonald Live Line Technology, MacDonald Mwakamele, alisema hakuridhika nayo kwa kuwa hakutilia maanani hoja alizoziwasilisha na kesho kampuni yake itafungua kesi katika Mahakama Kuu kuyapinga.

Alisema kuchelewa kwa kazi hiyo kulitokana na muda kuwa mfupi kwa kuwa zinapoagizwa nguzo Sao Hill inahitajika miezi mitano au sita zikauke pamoja na muda wa kuzisafirisha hadi eneo la mradi.

Alisema Tanesco ilimpa Sh milioni 400 wakati kazi ya kupata nguzo 700 na kuzisafirisha ilihitaji zaidi ya Sh bilioni moja na amejikuta katika hasara kutokana na nguzo alizoziaandaa kupelekwa eneo la mradi kuharibikia Sao Hill na nyingine kuibwa.

Alisema sababu nyingine iliyosababisha kuchelewa kwa kazi hiyo, ni meneja wa mradi aliyeteuliwa na Tanesco kutokuwahi kufika eneo la mradi huo.

Alisema alishangaa jinsi mkataba wake ulivyositishwa akisema aliandikiwa barua Desemba 1 hadi 2, 2010.

Barua ya kwanza ilimtambulisha kwa meneja mradi na ya pili iliitoa karipio la kusitisha mkataba.

Toa Maoni yako kwa habari hii

No comments: