Friday 24 January 2014

Bomani awashukia wanaobeza kazi ya Tume ya warioba

Mwanasheria Mkuu mstaafu, Jaji Mark Boman

Mwanasheria Mkuu mstaafu, Jaji Mark Boman amekitaka Chama cha Mapinduzi (CCM) kuachana na msimamo wake wa muundo wa Serikali mbili na kwamba, wawaachie wananchi waamue.

Pia, Jaji Bomani alisema anasikitishwa na madai yanayoelezwa na baadhi ya viongozi, tena anao waheshimu kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ni muumini wa Serikali tatu kwamba ni upuuzi, kwani yeye siyo wa kwanza kutaja muundo huo.

Licha ya hilo, alisema anashangazwa na baadhi ya viongozi kuwa rasimu imekwenda kinyume cha matakwa ya waasisi wa Tanzania na kwamba, kama hali inalazimu kubadili uamuzi unafanyika.

Akitoa maoni yake kuhusu Rasimu ya Pili ya Katiba, Jaji Bomani alisema licha ya kwamba yeye ni mwanaCCM, anaona Serikali tatu ni muhimu kwani ndiyo suluhisho la migogoro ya Muungano.

Alisema amekuwa mwanaCCM tangu mwaka 1960, lakini hajatetereka ingawa wakati mwingine amekuwa haridhiki na baadhi ya mambo.

“CCM ni chama tawala, chenye wanachama wengi kuliko chama kingine cha siasa, hivyo ina jukumu la kutoa uongozi na kuacha baadhi ya mambo wananchi waamue,” alisema Jaji Bomani na kuongeza:

“Nikisikia kitu kama wanaCCM kulishana kiapo ili wapinge Serikali tatu nafadhaika sana. Haya yote ya nini! Waachieni wanachama wenu waamue wanachokitaka kuliko kuwashinikiza kufanya uamuzi mnaotaka nyie.”

Alisema kazi ya chama ni kutoa ushauri na ushawishi, siyo kutoa shinikizo hivyo ni vyema kuacha kuwa na msimamao wa Serikali mbili, kwani kilichopendekezwa na Tume ndiyo sahihi.

Jaji Bomana alihoji kama CCM ilitaka Serikali mbili, iwapo waliwahi kuwapa wanachama wao elimu juu ya muundo huo.

“Itakuwa siyo uongozi bora kwa wana CCM kushinikiza kupigia kura mfumo wa Serikali mbili kwa namna ya vitisho. Nashauri wanachama na wananchi waachiwe uhuru bila kushinikizwa na mtu,” alisema Jaji Bomani.

No comments: