Thursday 23 January 2014

Chadema kutikisa nchi; Helikopta tatu kurushwa nchi nzima

Katibu Mkuu wa Chadema, Willibrod Slaa na mwenyekiti wake Freeman Mbowe wakielekea kuzungumza na waandishi wa habari, Makao Makuu ya chama hicho Dar es Salaam jana kuhusu kuanza kwa ‘Operesheni Pamoja Daima’ ya kuzunguka nchi nzima ili kuimarisha chama hicho

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuanzia leo, kinarusha helkopta tatu kwa siku 14 mfululizo, katika kutekeleza kampeni iliyopewa jina la Operesheni Pamoja Daima (ODB) itakayoendeshwa katika mikoa yote nchini.

Ziara hiyo inaanzia katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Ruvuma, huku viongozi wa chama hicho wakijigawa katika makundi sita; matatu yakitumia helkopta na matatu yatawafikia wananchi kwa kutumia usafiri wa magari.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa, lengo la operesheni hiyo ni kukiimarisha chama hicho na kuwafumbua macho wananchi kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.

“Tumejigawa katika makundi sita na makundi matatu kati ya hayo yatatumia helikopta kila moja, makundi mengine yatawafikia wananchi kwa misafara ya ardhini,” alisema Mbowe na kuongeza;

“Viongozi wakuu wa chama, wabunge, wenyeviti wa mikoa, wilaya, majimbo na kanda kila mmoja atashiriki kwa nafasi yake katika operesheni hii. Tutafanya mikutano kwa wiki mbili, ila tunaweza kuongeza wiki nyingine moja.”

Alisema chama hicho kimejipanga kuwafikia wananchi wengi kadri itakavyowezekana, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wake wa ndani kuanzia ngazi ya mashina, uchaguzi mdogo wa madiwani katika Kata 27 nchini utakaofanyika Februari 9, mwaka huu pamoja na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

“Naomba tueleweke, katika hili hatufanyi kampeni hata kidogo, huu ni mwendelezo wa maandalizi ya chaguzi mbalimbali. Kama mnakumbuka tulianza kujiandaa na uchaguzi wa mwaka 2015 baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010,” alisema Mbowe na kuongeza;

“Kwa sasa tunachokifanya ni kuongeza nguvu na umakini zaidi. Makundi yataanzia katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Ruvuma, tutapita kila Kata ambazo utafanyika uchaguzi wa madiwani.”

Mbowe alisema operesheni hiyo itapiga kambi katika Jimbo la Kalenga ambalo kwa sasa lipo wazi baada ya mbunge wake ambaye pia alikuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa kufariki dunia Januari 1, mwaka huu nchini Afrika Kusini.

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) haijatangaza kufanyika uchaguzi katika jimbo hilo, Chadema tutafika Kalenga na tutafanya mkutano maalumu na kutoa pole kwa wakazi wa jimbo hilo kutokana na msiba mkubwa wa mbunge wao,” alisema Mbowe.

Operesheni hiyo inafanyika siku chache tangu chama hicho kikuu cha upinzani nchini kipite katika mgogoro ambao ulisababisha aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe kukimbilia mahakamani ili kunusuru uanachama wake.

Wakati Zitto akinusurika kufukuzwa kutokana na zuio la mahakama, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo walifukuzwa uanachama, likiwa ni hitimisho la mchakato ulioanza kwa kuwavua nyadhifa zao pamoja na Zitto.

Daftari la wapigakura

Mbowe alisema msimamo wa chama chake ni kutaka daftari la kudumu la wapigakura lifanyiwe marekebisho kabla ya kupigwa kwa kura za maoni kwa ajili ya kupitisha Katiba Mpya.

“Tutagomea upigaji wa kura na tutawahamasisha wananchi kugomea kupiga kura. Serikali ya CCM isijidanganye kwa kuweka mikakati ya kukwamisha zoezi hili,” alisema Mbowe.

Alisema kama Serikali inataka amani iendelee kuwepo isifanye mzaha katika mchakato wa Katiba Mpya kwa maelezo kuwa Katiba siyo mali ya vyama vya siasa, bali ni mali ya wananchi.

“Katiba siyo ya Chadema, CUF wala NCCR-Mageuzi. Sheria inaeleza wazi kwamba daftari la wapigakura ni lazima lifanyiwe marekebisho mara mbili baada ya Uchaguzi Mkuu na kabla ya kuanza Uchaguzi Mkuu mwingine lakini hilo halijafanyika mpaka sasa licha ya Uchaguzi Mkuu kufanyika miaka minne iliyopita,” alisema Mbowe.

Alisema wapo Watanzania waliohama maeneo yao ya awali, waliopoteza vitambulisho, waliofikisha umri wa kupiga kura na kusisitiza kuwa kuwaacha watu hao nje ya mfumo wa kupiga kura ni kuwanyima haki yao ya Kikatiba.

“Kwa mujibu wa utafiti tulioufanya tumebaini kuwa wapo watu zaidi ya milioni 5 wanaohitaji kuingizwa katika daftari la wapigakura,” alisema Mbowe na kuongeza;

“Kama Katiba haitapita kwa sababu ya kutokuboreshwa kwa daftari la wapigakura hatutarudi katika Katiba ya sasa hiyo ni ndoto.”

No comments: