Friday 31 January 2014

DK slaa ndege ya kikwete tutaiuza

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willbrod Slaa, amesema chama chake kikiingia madarakani mwaka 2015 kipaumbele cha kwanza kitakuwa ni kuuza ndege ya rais ambayo inatumiwa na Rais Jakaya Kikwete, ili kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Katibu huyo alisema hayo juzi wakati akihutubia wananchi wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa mikutano ya M4C Operesheni Pamoja Daima.
"Kipaumbele kingine ambacho kipo katika ilani ya chama chetu ni kuhakikisha tunauza ndege ya Rais ya sasa iliyopo na kununua ndege itakayokuwa na uwezo wa kutua kila sehemu," alisisitiza Dkt. Slaa.
Alisema hatua hiyo inalenga kutatua changamoto zinazowakabili katika maeneo mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Dkt. Slaa alisema mishahara ya askari wenye vyeo vidogo ni midogo, hivyo haiwezi kukidhi mahitaji yao.
Alisisitiza kuwa mishahara ya askari hao imekuwa midogo sana kulingana na kazi wanazozifanya, huku posho zao za kila wiki zikiwa hazikidhi mahitaji yao kutokana na kuwa ndogo hali inayosababisha askari hao kushiriki vitendo vya rushwa.
Alisema jeshi la polisi limekuwa likijihusisha na vitendo vya rushwa kwa kuwakamata wauza gongo, pamoja na watu wenye dawa za kulevya kutokana na mishahara yao kuwa ya chini.
Alimtaka Mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP, Ernesti Mangu, kuhakikisha askari hao wanaachana na vitendo vya rushwa kwa kuwaongezea mishahara, pamoja na kuacha tabia ya kutumia kauli za kijeshi.
Aidha, Dkt. Slaa alibainisha kuwa Tanzania inakabiliwa na janga la kuwa na vijana wengi wa mitaani hali inayohatarisha maisha ya wananchi wengine kutokana na vijana hao kutokuwa na kazi yoyote, huku akilaumu Serikali kwa kushindwa kutatua kero hiyo.

No comments: