Friday 17 January 2014

Kipa namba moja wa timu ya Simba, Ivo Mapunda

kwa kifupi

Kiemba alikuwa na wakati mgumu wakati wa utawala wa kocha Abdallah ‘King’ Kibadeni kwani alikuwa akipangwa mara chache na mara nyingi alikuwa akisugua benchi huku ikidaiwa kuwa ameshuka kiwango jambo ambalo mwenyewe alilipinga.

KIPA namba moja wa Simba, Ivo Mapunda amesifu kiwango cha kiungo Amri Kiemba alichokionyesha katika michuano ya Kombe la Mapinduzi na kudai amewaziba midomo wote waliokuwa wakimbeza.

Kiemba alikuwa na wakati mgumu wakati wa utawala wa kocha Abdallah ‘King’ Kibadeni kwani alikuwa akipangwa mara chache na mara nyingi alikuwa akisugua benchi huku ikidaiwa kuwa ameshuka kiwango jambo ambalo mwenyewe alilipinga.

Wakati akiwekwa benchi Simba, kwa madai ya kushuka kiwango kiungo huyo alikuwa akianza katika kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ jambo lililozidi kuwashangaza wadau wa soka.

Hata hivyo, Kiemba aliwahi kusema yote yaliyokuwa yakimtokea kipindi hicho hawezi kuyazungumzia mpaka muda utakapofika.

Ivo aliliambia Mwanaspoti kuwa Kiemba ameonyesha kuwa anaweza kwani amekuwa msaada mkubwa kwa timu huku akipingana na kauli ya kocha wake Zdravko Logarusic ya kuanza kumchezesha mchezaji huyo kwa muda mfupi kwa madai ya umri.

“Ameonyesha kuwa anaweza kwani amecheza kwa kiwango cha juu sana na kuwa msaada mkubwa kwa timu mpaka hapo ilipofika na nafikiri wote waliokuwa wakimbeza wameona kiwango chake.

“Ila mimi nina mtazamo tofauti na mwalimu kwani sidhani kama ni sahihi alivyosema ataanza kumpumzisha kutokana na umri, mimi naamini bado anaweza sana na nafikiri wampumzishe mechi kadhaa ila zile muhimu lazima acheze kwani anajua sana,” alisema Ivo ambaye amesajiliwa na Simba kwenye dirisha dogo la usajili akitokea Gor Mahia ya Kenya.

Kipa huyo wa Taifa Stars alimtaka kiungo huyo azidishe mazoezi ili awe fiti na pia asiache kufanya sala ili Mungu aendelee kulinda kiwango chake.

No comments: