Friday 31 January 2014

Mbunge, Mkurugenzi nusura wazichape

Mbunge wa Viti Maalumu wa Chadema wa Mkoa wa Manyara, Paulina Gekul jana alilazimika kuokolewa na polisi wilayani hapa, kutokana na kushambuliwa na Mkurugenzi wa Halmashari ya Mji wa Babati, Omari Mkombole na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mohamedi Fara, wakigombea kabrasha lenye majina ya wanaopaswa kupewa ardhi.

Katika tukio hilo, Gekul ameeleza kuchaniwa nguo zake, kudhalilishwa na kuporwa fedha zaidi ya Sh5 milioni zilizokuwa kwenye mkoba wake.

Tukio hilo la kushambuliwa kwa mbunge huyo lilitokea juzi saa 12 jioni katika ukumbi wa halmashauri ya mji wa Babati, mara baada ya kikao kilichokuwa kikifanyika chini ya mkurungenzi huyo kumalizika.

Akizungumza mara baada ya kutoka polisi jana kutoa maelezo juu ya vurugu hizo, Gekul alisema kikao hicho kilichosababisha vurugu hizo, kilikuwa kinajadili mustakabali wa ugawaji wa shamba la Sisal Plantation lenye ekari 4200.

Alisema shamba hilo wakulima walilipia mwaka 2000 na Baraza la Madiwani lilikwishatoa uamuzi wa kugawanywa, lakini juzi katika orodha iliyotolewa, alibaini majina mengi yameghushiwa na walengwa wengi hawapo na baada ya viongozi wa halmashauri kubaini amegundua njama hizo, ndipo waliagiza kurejeshwa makabrasha yote.

“Mimi nilikataa kwa sababu orodha hii ina makosa na mimi nawafahamu baadhi ya wakulima wanaopaswa kupewa eneo hili “alisema Gekul.

Alisema Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mohammedi Fara

baada ya yeye kukataa kurejesha, aliahirisha kikao na walipotaka kutoka nje ghafla alitokea Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Omari Mkombole ambaye alidai alikwenda Polisi kufuatilia suala la wakulima hao na tayari wanataka kuendesha msako wa waliovamia eneo hilo bila idhini ya halmashauri.

“Lakini cha ajabu baada ya kusema hivyo, mkurugenzi huyu akanifuata na kunikaba kwa nguvu, kisha kunichania nguo zangu na kunipokonya karatasi akidhani zina majina ya wakulima hao,

Alisema baada ya mlango kufungwa alianza kupokonywa kwa nguvu pochi yake na wakachambua ndani na kuondoka na nyaraka zote, huku ufunguo wa gari ukitupwa.

Mkurugenzi wa Halmashauri Omari Mkombole, alipopigiwa simu ya mkononi ili kuzungumzia tukio hilo, hakupokea na simu yake iliita bila kupokewa, huku Mwenyekiti wa Halmashauri akikiri kutokea kwa vurugu hizo.

No comments: