Friday 17 January 2014

Mh.Mizengo Pinda ameagiza Tanroads kufanya upya tathmini ya ujenzi barabara Dodoma – Iringa.


Waziri mkuu Mh. Mizengo pinda ameuagiza wakala wa barabara nchini Tanroads kufanya upya tathmini ya ujenzi wa barabara ya Dodoma Iringa kwa kuweka miundombinu ya maji na madaraja yenye uwezo wa kupitisha maji kwa wingi ili kuepusha adha ya mafuriko kwa wakazi wanaoishi pembezoni mwa barabara hiyo.

Agizo hilo la waziri mkuu analitoa katika ziara ya kutembelea wahanga wa mafuriko zaidi ya 1400 ambao hivi sasa hawana mahala pa kuishi kufuatia kaya zaidi ya 140 kusombwa na maji katika kata za chipogoro na fufu baada ya maji ya mvua zinazoendelea kunyesha kujaa na kuathiri vijiji vinne vilivyoko pembezoni mwa barabara hiyo kutokana na kukosekana kwa madaraja ya uhakika na miundombinu ya kupitisha maji.

Awali wakitoa taarifa kwa waziri mkuu kuhusu mafuriko hayo mkuu wa wilaya ya Chamwino Fatma Aly ilipo kata ya Fufu na kaimu mkuu wa wilaya ya Mpwapwa Ernest Msovela ilipo kata ya Chipogoro wamesema mafuriko hayo kwa kiasi kikubwa yamesababishwa na ujenzi wa barabara hiyo ambayo haikuzingatia jografia ya maeneo hayo hasa kipindi cha mvua ambapo maji mengi hutiririka kutoka milimani

Nao baadhi ya wahanga wa mafuriko hayo wakaelezea changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo hivi sasa ambapo wamesema maisha yao yako hatarini kutokana na tishio la kukumbwa na magonjwa ya mlipuko.

Mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali ya mkoa wa dodoma tayari zimeaza kuleta madhara kutokana na mafuriko ambapo licha ya wakazi wa maeneo yanayokumbwa na janga hilo kukosa uhakika wa maisha lakini pia imeharibu miundombinu ya barabara sehemu mbalimbali pamoja na kusomba tuta la reli eneo la gulwe na godegode wilayani mpwapwa na kusababisha usafiri huo wa umma kusimama kwa muda usiojulikana

No comments: