Thursday 23 January 2014

Pigo jingine tena CCM, mbunge wa chalinze afariki dunia

MBUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jimbo la Chalinze, Said Bwanamdogo, amefariki dunia.
Akithibitisha taarifa za kifo cha Mbunge huyo Dar es Salaam jana, Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda, alisema kifo cha Mbunge huyo kilitokea jana asubuhi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu.
Alisema mipango ya mazishi inaendelea kufanywa na Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na familia ya marehemu. Mbunge huyo anatarajiwa kuzikwa leo kijijini kwake Miono wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Kifo cha mbunge huyo ni cha pili ndani ya mwezi, ambapo Januari 1, mwaka huu Mbunge wa Jimbo la Kalenga na aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Fedha, Dkt. William Mgimwa alifariki akiwa kwenye matibabu nchini Afrika Kusini.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Wilaya ya Bagamoyo, Ridhiwani Kikwete, lwa niaba ya CCM Wilaya ya Bagamoyo, kupitia mtandao wake wa jamii, alitoa pole kwa wapenzi,wanachama na mashabiki kwa kupoteza mbunge huyo.
" Tumepoteza Mbunge wetu , kipenzi chetu Saidi Bwanamdogo leo asubuhi, Naomba wote tuendelee kumuombea marehemu wetu apewe pepo na yote anayostahili," alisema Ridhiwani.

Kwa upande wa wabunge waliofanya kazi na marehemu huyo akiwemo Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi, alielezea kugusa na kifo na mbunge huyo na kusisitiza kuwa siku zote kifo chochote hakizoeleki.
"Mbunge huyo alikuwa mwanafamilia mwenzetu , tumepokea kwa mshtuko na majonzi makubwa taarifa za kifo chake," alisema na kuongeza; "Namfahamu kwa karibu hasa kwa kujenga na kutetea hoja za wananchi wa Chalinze na Tanzania kwa ujumla, hivyo ni pengo kubwa na wamelikubali kwa kuwa ni wito wa kila mmoja kwa Mungu.
Naye Mbunge wa viti maalum (CCM) kisiwani Pemba, Maua Daftari, amesema kifo cha Mbunge huyo ni pigo kwa taifa kutokana na kukubalika kwake kwa wananchi kwani alikuwa mpigania maendeleo.
Wakati huo huo,Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge, Anne Makinda, kutokana na kifo cha Mbunge wa Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bwanamdogo.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za kifo cha Mbunge wa Jimbo la Uchaguzi la Chalinze, hwa hakika kifo cha Mbunge huyu ambacho kimenigusa mno, si tu ni pigo kubwa kwa Bunge letu la alikokuwa akichangia kwa umahiri mijadala na hoja mbalimbali bali pia kwa wananchi wa Jimbo la Chalinze ambao alikuwa akiwawakilisha vyema na kwa uhodari mkubwa katika Bunge hilo,”alisema.
Rais Kikwete amemuomba Spika Makinda kumfikishia Salamu zake za rambirambi na pole nyingi kwa familia ya marehemu kwa kufiwa na baba, kiongozi na Mhimili madhubuti wa familia ambaye kwa hakika alikuwa tegemeo kubwa kwao katika kuiendesha vyema familia yao.
Hata hivyo, amesema hawana budi kuutambua ukweli kwamba kazi ya Mungu haina makosa.
Amewahakikishia wanafamilia, ndugu na jamaa wa marehemu Said Ramadhan Bwanamdogo kuwa, katika msiba huu, hawako peke yao kwani yeye binafsi yuko pamoja nao katika kipindi chote cha maombolezo na kwamba msiba huu ni wa wote.
Aliwaomba wanafamilia kuwa wavumilivu, watulivu, wenye subira na ujasiri ili waweze kuhimili machungu ya kuondokewa na kiongozi na mhimili wa familia. Habari zaidi ambazo zimefikia gazeti hili zilieleza kuwa Rais Kikwete, atashiriki mazishi wa mbunge huyo leo.

No comments: