Sunday 26 January 2014

TWIGA STAR inatia huruma jamani

TIMU ya soka ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ inacheza mechi yake ya kwanza ya mchujo wa kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake dhidi ya Zambia Februari 15 mwaka huu, lakini hali ya maandalizi ya timu hiyo inatia aibu.

Kocha wa timu hiyo, Rogasian Kaijage aliteua wachezaji 30 ambao wanaendelea na mazoezi yao kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam wakisubiri kuingia kambini keshokutwa Jumatatu kwenye kambi ya jeshi iliyopo Ruvu, Pwani.

Lakini kwa hali ilivyo kwenye timu hiyo tangu ianze mazoezi hakuna dalili yoyote ya umakini wa timu ya taifa inayojiandaa kwa mashindano.

Mpaka sasa benchi la ufundi limepwaya, halina kocha wa makipa licha ya umuhimu wa kocha huyo na badala yake makipa wenyewe ndiyo hupeana mazoezi baada ya kumaliza mazoezi yao ya kawaida.

Benchi hilo lina kocha mkuu na msaidizi wake, Nasra Juma ambaye mpaka sasa hajaanza kazi, daktari wa timu hiyo, Christine Lwambano, mtunza vifaa na meneja wa timu hiyo, Furaha Francis.

Mazoezi hufanyika Uwanja wa Karume, kila siku jioni lakini yamekuwa yakisuasua kwani si wachezaji wote wanaofika kwa muda unaopangwa kutokana na hali ya kiuchumi.

“Wachezaji wanatoka nyumbani, kuna shida ya usafiri na wengine huwezi kujua matatizo ya familia zao hivyo ni vigumu kumchukulia mchezaji hatua labda wangekuwa kwenye kambi ya pamoja, huwa nazungumza nao tu,” anasema Kaijage ambaye analalamika hajaridhishwa na hali ilivyo lakini hana jinsi.

“Ngoja tuone itakavyokuwa kwani tulitakiwa kuanza kambi mapema, niliwapa mapema programu yangu, haya mashindano ni makubwa na mchezo huo ni mgumu,” anasema Kaijage na kuongeza kuwa hata wachezaji wake hawafurahii hali inavyokwenda.

Nahodha wao, Sophia Mwasikili anasema: “Wanachoka ila tunajitahidi kuzungumza nao ili wasikate tamaa, mechi na Zambia ni ngumu lakini naamini tutaingia kambini wiki ijayo na tutafanya vizuri tu.”

Kipa namba moja wa kikosi hicho Fatuma Omary anayetoka timu ya Sayari Queens ndiye hupewa jukumu la kuwanoa makipa wenzake watatu Maimuna Seif, Belina Julius na Najiat Abbas kutokana na uzoefu wake ingawa bado wadau wamedai kwamba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) haliko makini na timu hiyo.

Daktari wa Twiga, Christine Luambano, anasema kwamba wachezaji wawili Flora Kayanda na Semeni Abeid ni wagonjwa hivyo watakuwa nje mpaka watakapopona.

“Flora anaweza kuanza mazoezi Jumatatu ila Semeni bado sana kidonda chake kitachukuwa muda kidogo.”Kipa Maimuna Said na Eto Mlezi ambao wote wanatoka timu ya JKT bado hawajaripoti mazoezini, bado hawajapewa ruhusa na mwajiri wao.

TFF haiweki wazi tatizo linaloikabili Twiga Stars zaidi ya kusisitiza kwamba lipo nje ya uwezo wao.

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura anasema: “Kambi ilitakiwa ianze Jumatano kama tulivyotangaza lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu tuliamua kuisogeza ila wataingia kambini.”

No comments: