Friday 24 January 2014

Waasi na serikali ya Sudan Kusini wasaini mkataba

Maelfu ya watu wameachwa bila makao kutokana na vita hivyo

Waakilishi wa serikali ya Sudan Kusini wanasema kuwa serikali imetia saini mkataba wa kusitisha vita na waasi.

Kulingana na mkataba huo uliotiwa saini mjini Addisa Ababa Ethiopia, mapiganao yanapaswa kusitishwa katika muda wa masaa 24.

Wapatanishi kutoka shirika la kikanda la IGAD, wamesema kuwa mkataba huo utatatua swala la kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa ambalo ndilo lilisababisha mazungumzo ya amani kukwama.

Aidha mkataba huo unatarajiwa kusitisha vita vya mwezi mmoja vilivyoanza tarehe 15 Disemba mwaka jana kati ya waasi na serikali.

Mazungumzo ya amani yamekuwa yakikumbwa na matatizo kuhusu swala la wafungwa 11 wa kisiasa ambao bwana Riek Machar anayeongoza waasi alitaka waachiliwe kama sharti la kutia saini mkataba wa amani.
Serikali yatwaa miji kutoka kwa waasi

Wiki jana wanajeshi wa serikali walifanikiwa kukomboa miji kadhaa iliyokuwa imetekwa na waasi.
Rais Obama

Jamii ya Kimataifa imeafiki mkataba wa kusitisha mapigano kati ya waasi na serikali ya Sudan Kusini uliosainiwa hiyo jana mjini Addis Ababa Ethiopia.

Marekani imesema, mkataba huo ni sehemu muhimu ya kurejesha amani na utawala wa sheria nchini Sudan Kusini.

Rais Obama ametaja kutiwa sahihi kwa mapatano hayo kama hatua muhimu ya kurejelea amani ya kudumu.

Hata hivyo Marekani imeonya kuwa mzozo huo bado haujatatuliwa na kutoa wito kwa pande zinazozozana kutekeleza mkataba huo mara moja.

''Tunatoa wito wa viongozi wa Sudan Kusini kuheshimu mkataba huo na kuhakisha kuwa mazungumzo zaidi kuhusu jinsi ya kutatua mzozo wa kisiasa unaokumba taifa hilo yanaendelea'' Alisema msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Mary Harf.

Zaidi ya watu 500,000 wamelazimika kutoroka makwao kutokana na vurugu hizo za mwezi mmoja.

No comments: