Saturday 18 January 2014

WATANZANIA KUCHEZESHA MECHI ZA CL, CC NA WASOMALI KUCHEZESHA YANGA, WACOMORO

Watanzania wanane wameteuliwa kuchezesha mechi mbili za marudiano za raundi ya awali za Ligi ya Mabingwa Afrika (CL) na Kombe la Shirikisho (CC) zitakazochezwa wikiendi ya Februari 14 na 16 mwaka huu.

Waamuzi hao walioteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ni Israel Mujuni atakayechezesha mechi ya CL kati ya Rayon Sport ya Rwanda na AC Leopards de Dolisie ya Congo itakayofanyika jijini Kigali.

Mujuni atasaidiwa na Josephat Bulali, Samwel Mpenzu na Ramadhan Ibada, wakati Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Jean Marie Hicuburundi wa Burundi.

Naye Waziri Sheha ataongoza jopo lingine kwenye mechi ya CC kati ya FC MK ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na El Ahly Atbara ya Sudan. Mechi hiyo itachezwa jijini Kinshasa.

Sheha atasaidiwa na Ferdinand Chacha, John Kanyenye na Israel Mujuni. Kamishna wa mechi hiyo ni Chayu Kabalamula kutoka Zambia.


WASOMALI KUCHEZESHA YANGA, WACOMORO

Shrikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Somalia kuchezesha mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga ya Tanzania na Komorozine Sports ya Comoro.

Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya mchujo itafanyika jijini Dar es Salaam kati ya Februari 7 na 9 mwaka huu wakati ile ya marudiano itachezwa kisiwani Comoro kati ya Februari 14 na 16 mwaka huu.

Mwamuzi wa kati atakuwa Hassan Mohamed Hagi wakati wasaidizi wake ni Hamza Hagi Abdi, Bashir Abdi Suleiman na Bashir Olab Arab. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Eugene Musoke kutoka Uganda.

Timu ambazo zimeingia moja kwa moja katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa ni Coton Sport ya Cameroon, El Ahly (Misri), TP Mazembe (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), El Hilal (Sudan), Club Sportif Sfaxien (Tunisia) na Esperance (Tunisia)

Nayo mechi ya kwanza ya raundi ya mchujo kati ya Azam ya Tanzania na Ferroviario Da Beira ya Msumbiji itakayofanyika Dar es Salaam kati ya Februari 7 na 9 mwaka huu itachezeshwa na waamuzi kutoka Sudan.

Waamuzi hao ni Mutaz Abdelbasit Khairalla atakayepuliza filimbi, Waleed Ahmed Ali, Aarif Hasab Elton na El Fatih Wadeed Khaleel. Kamishna wa mechi hiyo ni Hassan Mohamed Mohamed kutoka Somalia. Mechi ya marudiano itachezwa Msumbiji kati ya Februari 14 na 16 mwaka huu.

Timu zilizotinga moja kwa moja katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo ni Asec Mimosas ya Ivory Coast, Ismailia (Misri), Wadi Degla (Misri), Djoliba (Mali), MAS (Morocco), Bayelsa United (Nigeria), El Ahly Shandy (Sudan), E.S.S. (Tunisia), C.A.B. (Tunisia) na Zesco United (Zambia).

No comments: