Sunday 9 February 2014

Chadema ya itisha CCM

UCHAGUZI wa kata 27 za udiwani unaofanyika nchini leo unatarajia kutoa mwelekeo wa uimara wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

CHADEMA ambacho kimeonekana kukipa wakati mgumu CCM, kinaingia katika uchaguzi huo wiki moja baada ya kumaliza Operesheni ya M4C Pamoja Daima, iliyokuwa na lengo la kukiimarisha chama hicho na kutoa elimu juu ya Katiba mpya.

Uchaguzi wa leo pia unatarajia kutoa mwelekeo wa watu wanavyokiunga mkono chama hicho ambacho katika siku za hivi karibuni kiliamua kuwafukuza chamani aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo na Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Arusha, Samsom Mwigamba.

Pia CHADEMA ilimvua madaraka yote Naibu Katibu Mkuu (Bara), Zitto Kabwe, ambaye mpaka sasa amefungua kesi mahakamani akizuia uanachama wake usijadiliwe hadi rufaa yake anayokusudia kuikata katika Baraza Kuu la chama hicho.

Operesheni hiyo iliyafikia majimbo 166 na mikutano 206 iliyofanyika ilizua gumzo kubwa ndani na nje ya chama hicho kikuu cha upinzani, huku CCM wakikishutumu kwa kutumia fedha nyingi kukodisha helikopta tatu.

Hata hivyo CHADEMA waliweka wazi kuwa ufanisi wa operesheni hiyo ndilo jambo linalotishia uhai wa CCM ambayo kwa muda mrefu ilizoea kuviona vyama vya upinzani vikifanya harakati za kujiimarisha kila chaguzi zinapokaribia, lakini kwa CHADEMA hali imekuwa tofauti.

Katika uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 27 unaofanyika leo CHADEMA wanatetea kata mbili ambazo ni Nyasura iliyoko wilayani Bunda na Kiborloni iliyoko Moshi Mjini, huku zilizobaki ni za CCM.

Kwa upande wa CCM, uchaguzi huo utatoa taswira ya mapokeo ya wananchi juu ya utendaji usioridhisha wa mawaziri waliopachikwa majina ya ‘mizigo’ na viongozi wakuu wa chama hicho katika ziara zao walizofanya mwishoni mwa mwaka jana.

Kamati Kuu ya CCM ilipendekeza baadhi ya mawaziri wawajibishwe kwa kushindwa kuwajibika lakini Rais Jakaya Kikwete alipuuza ushauri huo alipofanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri hivi karibuni.

Kata zinazofanya uchaguzi pamoja na halmashauri zake kwenye mabano ni Segela na Mpwayungu (Chamwino), Ukumbi na Ibumu (Kilolo), Nduli (Iringa), Malindo (Rungwe) na Santilya (Mbeya).

Nyingine ni Tungi (Morogoro), Mkwiti (Tandahimba), Mkongolo (Kigoma), Sombetini (Arusha), Mrijo (Chemba), Magomeni na Kibindu (Bagamoyo), Mtae (Lushoto), Ubagwe (Ushetu) na Namikago (Nachingwea).

Kata nyingine ni Partimbo na Loolera (Kiteto), Kiwalala (Lindi), Kilelema (Buhigwe), Kiomoni (Tanga), Kasanga (Kalambo), Rudewa (Kilosa), Kiborloni (Moshi), Njombe Mjini (Njombe) na Nyasura (Bunda.

CUF watamba

Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Naibu Katibu Mkuu (Bara) wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, alisema chama chake kimejipanga katika maeneo mbalimbali walikosimamisha wagombea na wanatarajia kushinda katika kata husika.

Mtatiro alipuuza kauli iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kuwataka vijana wa chama hicho ‘Green Guards’ kuwa walinde wapiga kura, akisema hiyo ni kazi ya polisi.

CHADEMA

Nao CHADEMA wamesema wana uhakika wa kushinda kata zaidi ya kumi katika uchaguzi huo, huku wakitamba kuwa huko kutakuwa ni kuimega CCM, maana katika uchaguzi huu CCM ilikuwa na kata 25 ambazo leo inatarajia kuzitetea au izipoteze.

Akizungumza na waandishi wa habari, Makao Makuu ya CHADEMA, Mwenyekiti wa Bavicha, John Heche, alisema chama chake kitashinda kwa kishindo katika kata nyingi na CCM watarajie kushindwa vibaya katika uchaguzi huo.

Alibainisha kuwa alilaani kauli ya Nape, kwa kusema kuwa serikali imeshindwa kuwachukulia hatua viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na wafuasi wao ambao wanafanya kazi ya kuwateka viongozi na wafuasi wa CHADEMA sehemu mbalimbali nchini, hivyo amewataka vijana wa CHADEMA nao kulinda kura leo.

CCM watamba

Chama Cha Mapinduzi kupitia msemaji wake, Nape Nnauye, ameviomba vyombo vya dola na Tume ya Uchaguzi vitende haki.

“Uchaguzi huu sisi tutashinda, takwimu zinaonyesha kuwa tutashinda kata zote, lakini uchaguzi ni uchaguzi tu, sisi tutakubali matokeo yatakayotangazwa, ila tunaomba polisi na Tume ya Uchaguzi watende haki ili matokeo halali ndiyo yatangazwe,” alisema Nape.

Katika chaguzi ndogo zilizofanyika baada ya mwaka 2010, CHADEMA imekuwa ikipanda kwa kasi kwa kushinda katika kata na kupata kura nyingi katika chaguzi za majimbo ziliporudiwa.

Uchaguzi mdogo wa Igunga 2011, matokeo yalikuwa ni CCM kura 26,484 sawa na 47%, CHADEMA kura 23,260 sawa na 41%, CUF kura 2,104 sawa na 4%, AFP 282 sawa na 0.5% .

Wakati wa Uchaguzi Mkuu 2010, CCM Igunga ilipata kura 35,674, CUF kura 11,321, CHADEMA ilikuwa haina mgombea. Mwaka mmoja baadaye ilipata kura 23,260.

Mwaka 2012, matokeo ya uchaguzi mdogo Jimbo la Arumeru Mashariki, CHADEMA ilipata kura za Joshua Nassari 32,972, na kumshinda mpinzani wake mkuu katika uchaguzi huo, Sioi Sumari wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyepata kura 26,757.

Mwaka 2013, katika uchaguzi mdogo, CCM ilishinda kata 16 dhidi ya 22, CHADEMA ikashinda kata tano, muda mfupi kabla ya CCM kuambulia sifuri katika uchaguzi wa kata nne za Arusha ambazo CHADEMA ilishinda zote.

Uchaguzi huu wa leo, hata kama CHADEMA itapata kata zake mbili na kushinda nyingine moja itakuwa ni pigo kwa CCM, hivyo CHADEMA ikishinda kata nyingi zaidi itakuwa ni pigo kwa CCM, kwani itakuwa inaonyesha kuwa CHADEMA inashamiri na CCM inazidi kunyauka.

Arusha

Uchaguzi wa Kata ya Sombetini wilayani Arusha unatazamiwa kuwa na upinzani mkali kutokana na aliyekuwa diwani wa eneo hilo, Alphonce Mawazo, kuhamia CHADEMA na aliamua kutogombea.

Uchaguzi huu mdogo unavuta hisia za wakazi wengi wa jiji hili hasa kutokana na ushindani mkali uliopo baina ya wagombea wa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Ally Bananga na yule wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM), David Mollel, huku yule wa Chama cha Wananchi (CUF), Ally Mkali, akionekana kuwasindikiza wenzake.

Uchaguzi huu ni kipimo cha kukubaliwa na wananchi kwa vyama vya CHADEMA na CCM ambavyo vimekuwa vikuchuana ikiwa ni takriban miezi sita baada ya kumalizika kwa uchaguzi mdogo ambao CHADEMA waliibuka na ushindi kwenye kata zote nne zilizokuwa zikirudia uchaguzi ambazo ni Elerai, Themi, Kaloleni na Kimandolu.

Mchuano wa CCM na CHADEMA unazidi kuchagizwa na kutafuta kura ya maamuzi kwenye vikao vya baraza la madiwani kwani kwa idadi ya sasa ambayo CHADEMA wana madiwani 15 ndio wenye uwezo wa kufanya maamuzi, kwani CCM wako 14 na TLP wako 2.

Hivyo CHADEMA wakiibuka na ushindi kwenye uchaguzi wa leo ina maana wataendelea kuiongoza halmashauri hiyo kimaamuzi bila kulazimika kutafuta kuungwa mkono na madiwani wa chama kingine katika kupitisha hoja zao.

CCM ambao wana madiwani 14 kwa sasa wanahitaji kuongeza idadi hiyo ya kura ili kuwaongezea nguvu ya maamuzi kwenye vikao vya baraza hilo ambapo wakiwa na idadi sawa na CHADEMA wote watakuwa wakihitaji kuungwa mkono na TLP ili kuweza kupitisha jambo wanalokusudia.

Kampeni za uchaguzi zilitawaliwa na vurugu kiasi cha kuamuliwa njia maalumu zitakazotumiwa na wagombea na wafuasi wa vyama vya CHADEMA na CCM kwa ajili ya kwenda na kurudi kwenye mikutano yao ya kampeni kwani kila wanapokutana hutokea vurugu.

NEC yaonya

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva, aliwaonya viongozi wa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi kwenye Kata ya Sombetini kuacha kuchochea vurugu na badala yake wawahamasishe wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura.

Lubuva pia amelitaka Jeshi la Polisi mkoani hapa kutumia utashi na busara watakapokuwa wakiimarisha ulinzi wakati wa zoezi la upigaji kura kwenye kata hiyo ya Sombetini ili kuepuka kuwatisha wapiga kura.

Jaji Lubuva ameahidi kuongea na polisi ili awaombe wachukue tahadhari katika suala zima la kulinda na kuimarisha usalama ili wasitishe wapiga kura.

No comments: