Friday 14 February 2014

Kesi ya mauaji ya Mwangosi yanguruma tena

Dar es Salaam na Iringa. Kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi inayomkabili aliyekuwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mwenye namba G. 2573 Pacificus Cleophase jana ilianza kusikilizwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa.

Wakati kesi hiyo ikisikilizwa, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa mmoja kati ya 11 wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya kukusudia ya aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi, Longishu Losingo (29) amelalamika kuwa wanalishwa mchuzi wa maharage gerezani.

Kesi hiyo ya Mwangosi inasikilizwa na Jaji Mfawidhi, Mary Shangali.

Wakili wa Serikali, Adolf Maganda alidai kuwa mtuhumiwa Cleophase ambaye alikuwa askari polisi mkoani Iringa alifanya mauaji hayo Septemba 2 mwaka 2012 katika eneo la Nyololo, wilayani Mufindi.

“Mshtakiwa alitenda kosa hilo wakati alipokuwa akiwaamuru wafuasi wa Chadema kuondoka katika eneo la tukio walipopanga kufanyia mkutano,” alidai.

Maganda alidai kuwa katika tukio hilo, mtuhumiwa alifyatua risasi na kumpiga marehemu.

Wakili huyo alidai kuwa wafuasi wa Chadema walifika katika eneo hilo kwa ajili ya kuhudhuria mkutano ambao katibu mkuu wa chama hicho alikuwa anatarajia kuhutubia.

Alisema mkutano huo ulikuwa ufanyike licha ya polisi kuwaandikia Chadema ikiwataka wauahirishe ili kupisha zoezi la sensa.

Aliendelea kuieleza mahakama kuwa baada ya kuzuiwa kufanya mkutano, wafuasi wa chama hicho walianza kurusha mawe na kuwaumiza baadhi ya askari polisi, hatua iliyowalazimisha kuwatawanya kwa mabomu ya machozi na kwamba hatua hiyo ilikuja baada ya kuwasihi kutokufanya mkutano huo.

Maganda alidai kuwa mshtakiwa akiwa na bunduki alikwenda katika eneo la tukio alilokuwa marehemu na kufyatua risasi na kumpiga marehemu ambaye alikufa papohapo. Alidai kuwa taarifa ya daktari inaonyesha kuwa kifo cha Mwangosi kilisababishwa na kupatwa na majeraha yaliyotokana na mlipuko mkali.

Wakati kesi hiyo ikiendelea, katika hali isiyokuwa ya kawaida askari polisi walimkamata Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Iringa, Frank Leonard kwa madai kuwa alipiga picha mahakamani.

Baada ya kukamatwa, Leonard ambaye pia ni mwandishi wa Gazeti la Habari Leo na Daily News alifikishwa katika Kituo cha Polisi cha Kati na kuhojiwa kwa muda kabla ya kuachiwa Katika kesi ya Dk Mvungi, mshtakiwa alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Geni Dudu, ambapo aliwaomba watu wa haki za binadamu kuwatembelea gerezani ili waone jinsi wanavyoishi.

Alilalamika kuwa huko mahabusu wanalishwa maji ya maharage badala ya maharage.

Mshtakiwa alitoa malalamiko hayo, baada ya Wakili wa Serikali, Charles Anindo kuieleza mahakama kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi haujakamilika.

Imeandikwa na Berdina Majinge, Zainab Maeda na Tausi Ally

No comments: