Tuesday 18 February 2014

Ruvu Shooting yawapiga mkwara Wazee wa Uturuki

MAAFANDE wa Ruvu Shooting ya Pwani, wametamba kuendeleza wimbi la ushindi itakapokutana na mabingwa watetezi, Yanga ‘Wazee wa Uturuki’ katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara.

Timu hizo zitakutana Jumamosi Uwanja wa Taifa, jijini Dar
es Salaam huku Ruvu ikiingia uwanjani ikiwa na nguvu mpya kutokana na kushika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hivi sasa, baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union ‘Wazee wa Oman’ mwishoni mwa wiki na kufikisha pointi 25, ikiwa nyuma ya Simba kwa tofauti ya pointi saba.

Akizungumza kwa simu kutoka Kibaha mkoani Pwani jana, Ofisa Habari wa timu hiyo, Masau Bwire alisema, wanataka kuwadhihirishia mamilioni ya Watanzania kwamba, wana timu nzuri tofauti na inavyodhaniwa na wengi.

“Kwanza tunashukuru kuanza kutimiza malengo yetu, tangu mwanzo
tulitangaza tunataka ligi ikimalizika tuwe katika tano bora na hilo
limeanza kuonekana, sisi si Wacomoro (Komorozine), Yanga imecheza na timu sawa na timu ya kule nyumbani ya Mkulima SC, ndio maana ikashinda mabao mengi, mashabiki waje kwa wingi uwanjani kujionea kandanda safi la vijana wa Ruvu,” alitamba Bwire.

Alisema, Wacomoro ni timu ya kawaida sana na kuonya kuwa, mashabiki wa Yanga kama wanataka kujua ubora wa kikosi chao waanze kujipima kwa timu ngumu kama yao.

Aliongeza kuwa kutokana na maandalizi yaliyofanywa na Kocha wao, Tom Olaba, kwa sasa hakuna timu itakayowasumbua kutokana na wachezaji kumuelewa vema kocha wao.

No comments: