Thursday 13 February 2014

Soko la Kagunga Kigoma kunufaisha maziwa makuu

Ujenzi wa Soko la Kimataifa katika Kijiji cha Kagunga, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma mkoani kigoma jirani na mpaka wa Tanzania na Burundi linatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha kibiashara katika nchi za maziwa makuu.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Miriam Mmbaga amesema, ujenzi huo wa soko unatarajiwa kutumia Sh2 bilioni hadi kukamilika na litaongeza fursa za kiuchumi na kuchochea ukuaji wa ajira kwa wananchi wa nchi hizo tatu za Ukanda wa Maziwa Makuu.

Alisema bidhaa za uvuvi na kilimo ambazo zinazalishwa kwa wingi na wananchi katika maeneo hayo, zinatajwa kuwanufaisha wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa hawana soko la uhakika la kuuza bidhaa zao, badala yake huzisafirisha Burundi ambako soko lake halina uhakika.

“Licha ya biashara hizo za mazao ya kilimo na uvuvi, pia tunatarajia bidhaa nyingine za viwandani zitauzwa sokoni hapo, na jambo hilo litainua uchumi wetu kama halmashauri na taifa, kutokana na wananchi wetu kujipatia kipato sanjali na kukusanya ushuru na kodi za Serikali,” alisema Mmbaga.

Mkurugenzi huo ametaja changamoto ya ukosefu wa barabara inayokwenda kijijini hapo kama kikwazo kikubwa kinachokwamisha harakati za wafanya biashara kuwekeza kwa kasi katika soko hilo la aina yake mkoani hapa.

“Hakuna barabara inayounganisha Mji wa Kigoma na Kijiji hicho cha Kagunga,hii inafanya usafiri pekee unaotegemewa kuwa kwa njia ya boti katika Ziwa Tanganyika, ambapo mara kadhaa hutokea ajali ya kuzama, kitendo kinachofanya mali kupotea ziwani na nyingine kuharibika. Hii ni changamoto kubwa kwetu,” alisema Mmbaga.

Pia ufinyu wa bajeti inayopelekea ucheleweshaji wa mradi huo, ingawa kwa sasa wamepata mbia ambaye ni Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) ambao wanatarajia kutoa fedha za ujenzi huo zinazofikia Sh2 bilioni kwa ajili ya ukamilishaji wa mradi.

Ujenzi wa soko hilo ulioanza mwaka 2009 tayari umetumia Sh365 milioni kutoka mapato ya ndani ya halmashauri na kuna mkakati wa kutenga Sh500 milioni.

No comments: