Monday 31 March 2014

Kilimanjaro kuimarisha ulinzi katika nyumba za ibaada

KUTOKANA na tishio la vitendo vya kigaidi katika maeneo ya nyumba za ibada, Jeshi la Polisi Mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, limeanza mkakati wa kuweka ulinzi katika nyumba za ibada wakitumia dhana ya Polisi Jamii.
Akizungumzia mkakati huo kwa waumini wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Kristu Mfalme lililoko Moshi Mjini, mkoani humo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Moshi, (OCD), Deusdedit Kasindo, alisema lengo ni kujihami na matukio hayo kabla hayajatokea.
"Wenzetu katika nchi jirani, magaidi wamevamia Kanisa, kuua watu na wengine kujeruhiwa...nasi tumeona ni bora tukaanza kuchukua hatua kupitia dhana ya Polisi Jamii hivyo tunaomba ushirikiano wetu," alisema.
Aliongeza kuwa, kwa kuanzia jeshi hilo limetoa wito katika madhehebu mbalimbali wilayani humo kuanzisha vikundi vya ulinzi na usalama pamoja na kuviimarisha vilivyopo viweze kushirikiana na polisi kukabiliana na hali hiyo.
"Kumekuwa na vikundi vinavyojihusisha na wizi wa baiskeli, pikipiki na baadhi ya vitu ndani ya magari kwenye nyumba za ibada, lakini kwa hili la uvamizi ambao umeanza kushamiri hatuna budi kujiimarisha zaidi," alisema.
OCD Kasindo alisisitiza kuwa, tayari jeshi hilo limezunguka katika Makanisa na Misikiti mbalimbali mjini humo ili kutoa wito huo ambapo jeshi lipo tayari kutoa mafunzo yanayohusiana na ulinzi kama vikundi hivyo vitaundwa.
Alisema wameamua kusisitiza matumizi ya Polisi Jamii kutokana na jeshi hilo kuwa na askari wachache ukilinganisha na idadi ya wananchi wanaohitaji huduma za polisi maeneo mbalimbali.
"Matokeo ya sensa yaliyotoka hivi karibuni, askari mmoja ana jukumu la kulinda raia kati ya 1,300 na 1,500, hivyo ni muhimu raia wenyewe wakaanza kujichunga kwa asilimia 90 na asilimia 10 iliyobaki, usalama wao utasimamiwa na polisi," alisema.
Kwa upande wake, Paroko wa Parokia hiyo, Padri Crispin Jumanne, alilipongeza jeshi hilo kwa uamuzi huo uliokuja wakati mwafaka.
"Mkakati huu utasaidia kuwaondoa hofu waumini ambao baadhi yao walianza kuogopa na kushindwa kuhudhuria ibada...kwa niabaya Baba Askofu Isaack Amani, tunaahidi kutoa ushirikiano ambao tutauanza mara moja," alisema.
Alitoa wito kwa waumini wa kanisa hilo, kuliunga mkono jeshi hilo kwa kuwapa ushirikiano wao ili waweze kufanikisha azma ya kuhakikisha waumini wanafanya ibada kwa amani bila hofu.

No comments: