Friday 21 March 2014

Mtoto abakwa na kuuwawa kwa kuvunjwa shingo

MTOTO wa miaka 13, mkazi wa Kijiji cha Nyangoto Kata ya Matongo wilayani Tarime mkoani Mara (jina linahifadhiwa) amefariki baada ya kubakwa kisha kuvunjwa shingo na paja la mguu wake wa kulia.
Kamanda wa Mkoa wa Polisi Tarime/Rorya Justus Kamugisha, aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa tukio hilo lilitokea saa 6.30 mchana juzi.
Kamugisha aliongeza kuwa marehemu kwa mara ya mwisho alionekana akiongozana na mwanaume mmoja (jina tunalo) ambaye anadaiwa kutoroka baada ya kutenda tukio hilo. Alisema chanzo cha tukio hilo ni tamaa ya ngono.
"Mtoto huyo aligundulika akiwa tayari amekufa baada ya kubakwa na alikutwa amevunjwa shingo na paja la upande wa kulia,"alisema.
Juhudi za Jeshi la Polisi za kumtafuta mtuhumiwa ambaye alitoroka baada ya kutenda tukio hilo zinaendelea ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Nyangoto, Dkt. Kaijage Kagumilwa, alisema kuwa walipokea mwili wa marehemu saa saba mchana siku ya tukio.
Mwili wa mtoto huyo ulikutwa na majeraha mwilini. Dkt Kagumilwa alifafanua kuwa mtuhumiwa wa tukio hilo ana matatizo ya akili na kwamba ni ndugu wa karibu na marehemu.

No comments: