Sunday 27 April 2014

Afrika Kusini Yaadhimisha Miaka 20 ya Demokrasia

Wananchi wa Afrika Kusini wanasherehekea leo hii miaka 20 tangu kufanyika uchaguzi uliozishirikisha jamii zote za nchi hiyo katika uchaguzi uliomaliza utawala wa ubaguzi wa rangi.
Nelson Mandela akipiga kura mwaka 1994 Nelson Mandela akipiga kura mwaka 1994
Siku hiyo inaadhimishwa kwa maandamano mitaani, hotuba, sala, matamasha ya muziki na gwaride la kijeshi. Sherehe kuu itaongozwa na rais Jacob Zuma katika majengo ya Ikulu mjini Pretoria yajulikanayo ka Union Buildings, ambako viongozi wa serikali za ubaguzi walizitia saini sheria nyingi za kibaguzi ambazo rais wa kwanza mweusi wa nchini hiyo marehemu Nelson Mandela alizipinga karibu wakati wote wa uhai wake.
Siku hiyo ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia, tarehe 27 Aprili, 1994 imefanywa siku ya mapumziko, ikijulikana kama Siku ya Uhuru. Kwa raia wengi wa Afrika Kusini inaambatana na kumbukumbu ya furaha, wakati ambapo kwa mara ya kwanza watu weusi, wahindi, machotara na wazungu walichanganyika katika mistari mirefu mbele ya vituo vya kupigia kura.
Matumaini sambamba na kukata tamaa
Raia wengi weusi walifurahia uhuru baada ya miongo mingi ya ubaguzi wa rangi Raia wengi weusi walifurahia uhuru baada ya miongo mingi ya ubaguzi wa rangi
Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel askofu mstaafu Desmond Tutu amesema siku hiyo ilikuwa na mihemko ya mapenzi, huku rais wa mwisho wa serikali ya kibaguzi, FW de Klerk ameielezea kuwa siku ya fahari kuu kwa Afrika Kusini.
Hata hivyo, miaka 20 baadaye, msisimko huo umemalizika, na watu wanakitathmini kipindi hicho cha utawala wa demokrasia kuwa chenye mchanganyiko wa mafanikio na kushindwa.
Miongoni mwa mambo mengine, Afrika Kusini inajivunia katiba ambayo ni mojawapo ya bora kabisa duniani, mahakam huru na kuwa nchi ambayo pengine inaongoza kiuchumi barani Afrika. Lakini mafanikio hayo yametiwa doa na matumizi mabaya ya fedha za umma na lawama za ufusadi zinanoelekezwa kwa viongozi wa chama Tawala-ANC.
Changamoto zinaongezeka
Askofu Desmond Tutu ambaye anazingatiwa kuwa Nuru ya uadilifu nchini Afrika Kusini, ameelezea miongo miwili iliyopita kama kipindi cha mafanikio makubwa, lakini anaapa kuwa hatakiunga mkono chama cha ANC katika uchaguzi mkuu ujao.
Licha ya mafanikio makubwa, bado umaskini ni tatizo sugu nchini Afrika Kusini Licha ya mafanikio makubwa, bado umaskini ni tatizo sugu nchini Afrika Kusini
Maadhimisho haya ya miaka 20 ya uhuru yanafanyika katika mwaka ambamo pia kuna uchaguzi mkuu, tarehe 7 Mei. ANC inatarajiwa kushinda uchaguzi huo wenye ushindani mkubwa, licha ya shutuma ubadhirifu na kupanuka kwa pengo kati ya matajiri na maskini ambavyo vilishuhudiwa chini ya utawala wake.
Kuendelea kupendwa kwa chama cha ANC ni ushahidi kwamba wananchi wengi wa Afrika Kusini wanahisi hali ni bora zaidi ikilinganishwa na wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi ulioendeshwa na wazungu walio wachache nchini humo.
Mazingira bora ya maisha
Serikali imeamua kuadhimisha miaka 20 ya uhuru chini ya kauli mbiu isemayo, ''Afrika Kusini-mahali bora pa kuishi''.
Katika kipindi hicho, uchumi umeongezeka mara tatu, na serikali imesema imejenga nyumba zipatazo milioni 3.7, kwa watu ambao hapo nyuma hawakuwahi kuishi katika nyumba za kisasa. Vile vile, watu milioni 15 katika ya milioni 51 wa nchi hiyo wanapokea msaada wa serikali.
Raia wengi weusi sasa wanao uhuru wa kuishi na kufanya kazi watakako katika nchi yao, na weusi ambao wanahesabiwa katika daraja la kati wameongezeka sana.
Hata hivyo bado kupishana kwa kipato kumewafanya maskini wengi kuandamana mitaani, wakilalamikia ukosefu wa huduma za msingi kama vile maji safi, umeme na makazi. Na Afrika Kusini bado ni miongoni mwa nchi zenye pengo kubwa sana kati ya matajiri na maskini.

No comments: