Friday 11 April 2014

Okwi aipanikisha yanga

BONGO kwa sasa kuna timu nne ambazo zinalipa wachezaji mishahara ya maana. Kuna Yanga, Simba, Azam na Coastal Union. Lakini timu zote hizo na wachezaji wote unaowajua wachezaji huko hakuna ambaye anakula mkwanja mkubwa kama Emmanuel Okwi wa Yanga.

Jamaa anapiga Sh6.4 milioni. Sasa ameibua utata mwingine ndani ya Yanga ambao umemlazimisha kocha wake kumchimba mkwara mzito. Imebainika kwamba Okwi haumwi chochote kama baadhi ya viongozi wanavyosisitiza.

Mmoja wa vigogo wazito wa Shirikisho la Soka la Uganda (Fufa), ambaye ni swahiba mkubwa wa mchezaji huyo aliyesusa kuzungumza chochote, alisema alimwambia kwamba Yanga wamekiuka mkataba wake ndio maana akasusa.

Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu, anadai kwamba Okwi hayupo katika kikosi hicho kutokana na kupata maumivu ya goti lakini daktari wa timu hiyo, Juma Sufiani, ambaye alisema hana taarifa zozote za kuugua kwa mchezaji huyo aliyeigharimu Yanga na kusema kutokuwapo kwake uwanjani kunatokana na matatizo ya kiutawala ambayo hayajui wala hayamhusu.

Sufiani alisema katika faili lake kulikuwa na wagonjwa wawili tu ambao ni kiungo Haruna Niyonzima na beki David Luhende ambao hata hivyo wameshapona na jana Alhamisi jioni waliotarajiwa kuanza mazoezi na wenzao kabla ya kuanza safari leo Ijumaa alfajiri kuelekea Arusha kuifuata JKT Oljoro.

“Binafsi sina taarifa za kuumwa kwa Okwi, kutokuwepo kwake kwenye timu siyo kwa sababu za kitabibu, ni matatizo ya kiutawala zaidi ambayo siyajui wala hayanihusu, ” alisema Sufiani ambaye ni daktari wa zamani wa Taifa Stars na Kilimanjaro Stars.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, ambaye alinogesha filamu hiyo kwa kusema tangu walipomaliza mchezo dhidi ya Mgambo JKT wiki moja iliyopita na kuanza maandalizi ya mchezo uliofuata, Okwi hakuonekana tena katika mazoezi huku akisisitiza watafutwe viongozi ambao ndiyo wana majibu ya jambo hilo.

“Hatuna taarifa za kuumwa kwa Okwi, tunasikia tu anaumwa mara ya mwisho tulikuwa naye Tanga alipocheza mchezo dhidi ya Mgambo, alicheza vizuri na hakuwa na maumivu yoyote, sijui hayo maumivu ya goti yamemuanza lini na aliyapata katika mchezo gani,” alisema Mkwasa ambaye ni miongoni mwa makocha wasomi wa Tanzania.

Juhudi za kumtafuta Okwi zilifanyika kwa kiwango cha kutosha lakini mchezaji huyo hakutoa ufafanuzi. Kocha Pluijm alisema; “Siwezi kumzungumzia mchezaji asiyekuwapo pamoja na timu, suala lake waulize viongozi wa juu ndiyo wanaoweza kulizungumzia kwa undani.

“Katika timu yangu hana nafasi ya kucheza, hata kama akija kambini siku mbili au moja kabla ya mchezo hatapata nafasi kwa sababu hajafanya mazoezi ya pamoja muda mrefu. Siyo huyo peke yake hata hao wengine, mchezaji asiyefanya mazoezi ya pamoja na timu kamwe sitampa nafasi.”

Okwi alikuwapo jukwaani Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi Jumatano akifuatilia mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar ambayo Yanga ilishinda mabao 2-1, lakini aliondoka robo saa kabla ya mechi hiyo kumalizika.

No comments: