Saturday 26 April 2014

Okwi atimka kimya kimya

Emanuel Okwi akisubiria nyaraka zake kukaguliwa ili aweze kuanza safari yake ya kuelekea Uganda                            
 WACHEZAJI wa Yanga washambuliaji Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza wameondoka jana Jumatano jijini Dar es Salaam lakini cha kushangaza ni usiri wa safari yao.
Okwi ambaye hadi anaondoka jana saa tatu usiku alikuwa katika mgomo wa kutoichezea timu yake kutokana na madai ya fedha kiasi cha dola 40,000 (Sh 64 milioni) ndiye alikuwa wa kwanza kufika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akimtangulia Kiiza.
Mara baada ya kumuona mwandishi wa Mwanaspoti huku akipigwa picha za kutosha alionekana kushangazwa akiuliza nani ametoa siri ya safari yake.
Akiwa katika mshangao kuhusu kuvuja kwa siri ya safari yao ya usiku, Okwi ambaye aliletwa na gari aina ya Noah yenye namba za usajili T367 CJC alisema kwa kifupi kwamba anaondoka akirudi kwao Uganda kupumzisha akili yake kufuatia msimu wa Ligi Kuu Bara kumalizika.
Hata hivyo aligoma katakata kueleza undani wa mgomo wake ingawa Mwanaspoti lina uhakika kwamba anaidai Yanga fedha hizo ikiwa ni mabaki ya dau lake la usajili na hajalipwa.
“Nani amewaambia naondoka saa hizi? Hebu nitajie, Ok kifupi narudi nyumbani kupumzika ligi imekwisha hilo ndilo ninaloweza kusema, nimechelewa jamani naomba mniache nitaachwa na ndege,” alisema Okwi.
Na ingawa alificha kinachoendelea kati yake na Yanga, mmoja wa rafiki zake ameliarifu Mwanaspoti kuwa mchezaji huyo ameondoka lakini hajamalizana na uongozi wa klabu hiyo ambao umemuwekea ngumu kummalizia fedha zilizosalia huku akidaiwa kushindwa kuonyesha uwezo uliotarajiwa katika kipindi cha miezi sita ya usajili wake.
Dakika 20 baadaye Kiiza naye alitua uwanjani hapo na alipoulizwa kuhusu kuondoka kwake alisema anarudi kwao lakini hajajua siku ya kurudi.
“Foleni zimenimechelewesha jamani, narudi nyumbani ligi imekwisha nakwenda kupumzika ingawa nitakuwa na timu ya Taifa ya Uganda, sijui nitarudi lini kutokana na ratiba ya mechi za timu ya taifa,” alisema Kiiza.

No comments: