Tuesday 15 April 2014

Simba yaiendea Yanga Zanzibar

TIMU ya Simba inatarajia kuwasili kisiwani hapa leo kwa ajili ya kuweka kambi ya matayarisho ya kujiaanda na mchezo wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga utakaochezwa Aprili 19, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Simba, Abdul Mshangama alisema lengo la timu hiyo ni kujiandaa kikamilifu kukabiliana na Yanga katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu ya Vodacom unaotarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Alisema ujio huo utakaokuwa na wachezaji 20 watakaoshuka dimbani siku hiyo, wanatarajia kufanya mazoezi katika Uwanja wa Amaan saa za jioni
"Kutokana na umuhimu wa mchezo huo wa Simba na Yanga, tumeamua kuweka kambi Zanzibar ambapo tunaona ni sehemu pekee itakayotusaidia tufanye vizur siku hiyo, ambapo kutakuwa na ushindani mkubwa dhidi ya timu hizi mbili," alisema Mshangama.
Alisema pia watacheza mechi moja dhidi ya timu ya Malindi ambayo inashiriki Ligi Kuu ya Zanzibar, ikiwa ni kuichangia timu hiyo kwa kifo cha daktari wa Malindi, Abdallah Salungi kilichotokea mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu.

No comments: