Saturday 26 April 2014

Tunaweza Lierpool

MERSEYSIDE, LIVERPOOL
KAMA Barrack Obama alivyowaambia Wamarekani katika harakati za kampeni za uchaguzi wao mwaka 2008 kuwa wanaweza kumaliza matatizo yao, ndivyo kocha, Brendan Rodgers, alivyowaambia mashabiki wa Liverpool kuwa wanaweza kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England.
Juzi Jumapili usiku, harufu ya ubingwa wa ligi hiyo ilianza kunukia katika viunga vya Anfield huku pia mashabiki wengine wa timu hiyo duniani wakianza kuingiwa na kiwewe baada ya Liverpool kuichapa Tottenham mabao 4-0.
Wana nafasi kubwa ya kuwa mabingwa kama wakishinda mechi zao sita zilizobaki ambapo mbili kati ya hizo watacheza na wapinzani wao katika mbio hizo Chelsea na Manchester City.
Rodgers ana uhakika kuwa timu yake hii ina uwezo mkubwa wa kuhimili presha na kutwaa ubingwa hasa katika kipindi hiki ambacho wanaongoza msimamo wa ligi hiyo.
“Bado kuna pointi nyingi za kuzisaka na lazima kuna pointi zitakazopotezwa na timu zote kabla ya mwisho wa msimu. Hatuna presha yoyote na tuna uhakika kwa jinsi tunavyocheza,” alisema Rodgers ambaye alitua Anfield akitokea Swansea.
“Ndoto ya mashabiki wetu ni kutwaa ubingwa. Imekuwa muda mrefu sana tangu walipotwaa, lakini mimi haipo katika mawazo yangu. Tunahitaji kujiandaa tu na kufanya vizuri na kama tukifanya hivyo tutashinda mechi zetu.
“Chelsea na Manchester City wanajua kwamba Anfield itakuwa sehemu ngumu kuja. Tunapenda kucheza hapa, tunapata sapoti kubwa na hilo linasababisha tuongeze ari. Tunawaheshimu Chelsea, wana kocha wa kiwango cha juu sana na wana timu ambayo wameikusanya kwa ajili ya kushinda Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu.
“Manchester City ni miongoni mwa wababe wapya wa soka duniani, lakini tunadhani tunaweza kushinda mechi yoyote kwa sababu sisi ni timu. Tuna njaa na mbinu zetu za kisoka zinaimarika kila siku.”

No comments: