Sunday 13 April 2014

Urusi ya puuza vitisho vya marekani

Urusi. Vita ya maneno kati ya Urusi na nchi za Magharibi inaendelea kuchukua sura mpya baada ya Urusi kusema wazi wazi kwamba haibabaishwi na vitisho vya Marekani.

Kauli ya Urusi imekuja baada ya Marekani kuionya Moscow iache mpango wake wa kununua mafuta Iran. Urusi imefanikiwa ‘dili’ lake la kununua mapipa 500,000 ya mafuta kwa siku nchini Iran jambo ambalo Marekani ana wasiwasi litasaidia kukuza mpango wa nyuklia wa Iran.

Naibu Waziri wa Masuala ya Nje wa Urusi, Ryabkov anaeleza kwamba biashara yake na Iran ni suala la kawaida ambalo halihusishi masuala yoyote ya kisiasa wala changamoto za kiuchumi.

Katika makubaliano ya awali yaliyofanywa na nchi za Magharibi ikiwamo Marekani kuanzia kipindi cha Januari mpaka Julai, mwaka jana, Iran ilitakiwa kuuza nje ya nchi hiyo mapipa milioni 1 tu kwa siku.

Nchi ambazo Iran inatakiwa kuuza mafuta yake ni; China, India, Japan, South Korea, Taiwan na Turkey. Urusi haipo kwenye makubaliano hayo lakini sasa imeingia kwenye ‘dili’ kubwa ya kufanya biashara hiyo.

Mzozo kati ya Urusi na Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya (UN), unaendelea kushika kasi hasa baada ya Urusi kusogeza majeshi yake mpakani mwa Ukraine hivi karibuni.

Wakati Urusi ikisogeza majeshi yake karibu na Ukraine dunia haikujua alikuwa na lengo gani, lakini baada ya siku chache wananchi wa Crimea walipiga kura na kujiunga na Urusi.

Baada ya wananchi wa Crimea kujiunga na Urusi, wananchi wengi wa Mashariki mwa Ukraine nao sasa wameanza vuguvugu la kutaka kujiunga na Urusi.

Wananchi hao wameanza maandamano kwa wiki mbili sasa na wameshikilia majengo kwenye miji mitatu mikubwa ya Kharkiv, Luhansk na Donetsk ambayo ipo Mashariki mwa Ukraine na kuchoma matairi barabarani wakishinikiza kupigwa kwa kura ya maoni kama wenzao wa Crimea na kujiunga na Urusi.

Kutokana na kuwapo kwa vurugu hizo Marekani imetoa kauli kali kwa Urusi kwamba iache mikakati yake ya kuigawa Ukraine vipande vipande.

Kabla ya kutolewa kwa kauli hiyo Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) zimekuwa zikijiandaa kuiwekea vikwazo Urusi kutokana na kulichukua Jimbo la Crimea. Vikwazo vya awali vilivyowekwa ni kuzuia baadhi ya maofisa wa Urusi kusafiri katika nchi za Ulaya na Marekani. Majadiliano zaidi yanaendelea kuiwekea Urusi vikwazo zaidi.

Wakati Marekani ikitoa kauli hiyo na ikijiandaa kuiwekea vikwazo zaidi Urusi, serikali ya Ukraine imetoa saa 48 kwa wananchi wanaoshinikiza kujiunga na Urusi kuamua kubaki Ukraine la sivyo serikali hiyo itatumia nguvu kuwatawanya waandamanaji hao na kutupilia mikakati yao.
Kutokana na kauli hiyo Rais wa Urusi, Vladmir Putin ameionya Ukraine kuacha makosa ya kutumia nguvu kwani uamuzi huo utaigharimu.

Wakati mvutano mkali wa kisiasa ukiendelea kati ya Urusi na nchi za Magharibi, inaonekana hivi sasa Urusi amehamishia mikakati yake ya kupambana na nchi za Magharibi kwenye masuala ya kiuchumi.

Mapema mwezi huu, Urusi imepandisha bei ya gesi mpaka Dola 485 za Marekani meta za ujazo 1,000 kutoka Dola 268.50 za Marekani. Vilevile Moscow wanaidai Ukraine zaidi ya Dola 2.2 bilioni za Marekani

Wakati serikali ya Urusi ikipanga kufanya hivyo, Rais Vladimir Putin amelitaka baraza lake la mawaziri lisichukue hatua yoyote mpaka watakapofanya mazungumzo na nchi za Ulaya ikiwamo Ukraine.

Kutokana na deni hilo Ukraine inasema kwamba iko tayari kulipa, Dola 2.2 bilioni za Marekani, lakini kwa awamu. Asilimia 15 ya gesi inayosambazwa Ulaya kupitia Ukraine, inatoka Urusi na Ukraine inatumia nusu ya gesi hiyo.

Mvutano huo wa kiuchumi na kisiasa, sasa Ukraine ipo tayari kununua gesi kutoka nchi nyingine.

Mchambuzi wa masuala ya kiuchumi wa Kiev nchini Ukraine Alexander Paraschiy anasema: “Kama Poland na Hungary wataanza kusambaza gesi mapema kama ilivyokuwa mwaka jana, Ukraine itakuwa katika hali nzuri na Ulaya haitakabiliwa na tatizo la nishati ya gesi.”

Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi Kanda ya Ulaya wanasema kuwa Rais Putin, anatumia gesi kama fimbo ya kuibana Kiev ili isikubaliane na sera za Umoja wa Ulaya (EU) kuhusu masuala ya kiuchumi.

No comments: