Saturday 26 April 2014

wawili mbaroni kwa mauaji ya mwanafunzi

JESHI la Polisi mkoa wa kusini Pemba, linawashikilia vijana wawili marafiki wa karibu wa marehemu  Mohamed Soud Makame (17),  wakidaiwa kuchangia  mauaji yake.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Juma Yuuf Ali, alisema vijana hao wenye umri wa miaka 17 na 21 walishawishika kuwahoji kutokana na ukaribu waliokuwa nao na marehemu kabla ya kifo chake.

Alisema vijana hao wote walikamatwa wakiwa nyumbani kwao shehia ya Wawi wilaya ya Chake Chake na mara watakapomaliza kuwahoji wakihisi wanahusika na kifo cha marehemu huyo watafikishwa mahamani.

Hivyo aliwataka ndugu na jamaa wa marehemu huyo, kuwa watulivu na wastahamilivu, wakati huu jeshi la polisi likendelea na uchunguzi ili haki itendeke.

“Sisi Jeshi la polisi kwetu ni kuwataka wananchi na hasa ndugu na jamaa wa marehemu Mahamed Soud Makame, kuwa wastahamilivu na kutoa ushirikiano na jeshi letu, ili liweze kukamilisha kazi yake kwa ufanisi,’’ alisema.


Katika hatua nyengine Kamanda huyo,alisema juzi mara baada ya kutokezea kifo hicho,  kwa hatua za awali walibaini marehemu alifanyia ukatili kwa kuuliwa eneo la mbali na kisha mwili wake kufikishwa kwenye nyumba ambayo haijahamiwa.

“Unaweza kusema kuwa kifo chake sio cha kawaida, maana uchunguzi wetu ulibaini kuwa alikuwa na michubuko sehemu mbali mbali za mwili wake na wala hakuuliwa kwenye eneo ambalo tulimkuta bali pale aliletwa akiwa ameshakufa,” alisema.

Daktari Ali Hamran Mohamed wa hospitali ya Chake Chake, alieufanyia uchunguuzi mwili wa marehemu, alisema inaonesha kifo chake kilisababishwa na kuekewa kitu kizito shingoni, mithili ya kamba na kusababisha ulimi kutoka nje.

No comments: