Saturday 17 May 2014

Chama cha BJP chashinda uchaguzi India


Waziri mkuu mteule nchini India Narendra Modi

Kuna mwamko mpya wa kisiasa nchini India ambapo chama cha kitaifa cha Hindu ,BJP kimeshinda uchaguzi uliokuwa na maamuzi makali kuwahi kufanyika nchini humo kwa kipindi cha miongo mitatu.
Chama cha Congress ambacho kimelitawala taifa hilo kwa kipindi kirefu cha miaka 67 tangia uhuru wa taifa hilo kilishindwa vibaya.
Huku kikiwa na idadi kubwa ya wabunge,chama cha BJP sasa kina uwezo wa kutawala taifa hilo bila ushirikiano na chama chochote.
Wakati huohuo rais Barrack Obama wa Marekani amemkaribisha mjini Washington waziri mkuu mteule wa India Narendra Modi kufuatia ushindi mkubwa wa chama chake.
Rais Obama alimpigia simu kiongozi huyo akisema kuwa anatarajia ushirikiano wa karibu mbali na kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.
Kabla ya uchaguzi huo,Marekani ilikuwa imekataa kumpa viza ya kuingia nchini humo bwana Narendra Modi kufuatia ghasia dhidi ya waislamu katika jimbo analotoka la Gujarati mnamo mwaka 2002.
lakini wizara ya maswala ya kigeni nchini Marekani imesema kuwa kiongozi huyo hatakabiliwa na vikwazo vyovyote kwa kuwa kama kiongozi wa serikali atapewa viza maalum.
Baadhi ya viongozi waliompigia simu ili kumpongeza waziri huyo mteule ni waziri mkuu nchini Uingereza David Cameron,waziri mkuu nchini Pakistan Nawaz Sharrif pamoja na mawaziri wakuu kutoka Israel na Australia.

No comments: