Thursday 22 May 2014

Samatta na Ngassa Kushindania Tuzo moja

Samatta na Ngassa
Mchezaji wa Yanga, Mrisho Ngassa pamoja na Mbwana Samatta wa TP Mazembe, wanaumana katika kuwania tuzo za mwanamichezo anayependwa zaidi na watu zinazoendeshwa na Kampuni ya Bongo 5 Media Group kupitia tovuti yake ya bongo5.com.
Wengine wanaowania tuzo katika kipengele hicho ni Ramadhan Singano (Simba SC), Juma Kaseja (Yanga) na bondia Francis Cheka.
Inaonekana kuwa Ngasa na Samatta watakuwa na ushindani mkubwa zaidi hasa ikizingatiwa kuwa wachezaji wote wana mashabiki wengi na pia kila mmoja anacheza mchezo unaopendwa na wengi.
Akizungumzia tuzo hizo, mhariri mkuu wa bongo5.com, Fredrick Bundala, alisema watu wengi walijitokeza kupigia kura kuchagua watu wanawataka kushinda tuzo mbalimbali.
Bundala alivitaja vipengele vingine na majina ya waliopendekezwa kuwa ni pamoja na Nisher, Adam Juma, Nick Dizzo, Mecky Kaloka, Jerry Mushala wanaowania tuzo ya Mwongozaji Bora wa Video za wasanii.
Video Bora kwa Wanaume ni My Number ya Diamond, Jikubali ya Ben Pol, Mirror ya Baby, Love Me ya Izzo Bizness, Barnaba na Shaa, Muziki Gani ya Nay wa Mitego na Diamond.
Alisema wanaowania Tuzo ya Video ya Mwanamuziki wa Kike ni Amani ya Moyo ya Feza Kessy, Closer ya Vanessa Mdee, Sugua Gaga ya Shaa, Yahaya ya Lady Jaydee, Nakomaa na Jiji ya Shilole.
Bundala alifafanua kuwa wananchi wanatakiwa kuchagua jina moja kutoka katika majina matano ya kila kipengele kilichotajwa.
“Wiki moja baada ya majina ya washiriki watano kutangazwa, mchujo wa kwanza utafanyika katika kila kipengele,” alisema Bundala.
Aliwataka Watanzania kuwapigia kura wale wanaowapenda kwa kutuma ujumbe mfupi na baadaye kufuata maelekezo rahisi ya kupiga kura pia kupitia tovuti www.tuzozetu.com.

No comments: