Thursday 15 May 2014

Tunalenga usaidizi wa kibinadamu CAR na kuwezesha jamii kujikwamua; OCHA

Wananchi wa CAR wakikumbatiana baada ya kuwasili salama Sido, mpaka mwa Chad akitokea Bangui.
Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR,  hali ya usalama inayozidi kuzorota kila uchao imesababisha uchumi nao kuendelea kuporomoka ambapo Umoja wa Mataifa umesema unaweka vipaumbele vya usaidizi kwa kuzingatia rasimu ya mpango ulioandaliwa na serikali ili kukwamua nchi hiyo. Ripoti kamili na Alice Kariuki.
(Taarifa ya Alice)
Uimarishaji wa ulinzi na usalama, utawala bora, usaidizi wa kibinadamu na maendeleo ya kiuchumi, hayo ni mambo manne ambayo Ofisi ya Umoja huo inayohusika na usaidizi wa kibinadamu, OCHA imetaja kuzingatia katika operesheni zake.
OCHA imesema watu Milioni Mbili na Nusu nchini humo ambao ni zaidi ya nusu ya wakazi wa nchi hiyo sasa wanahitaji usaidizi kwani shughuli za kujipatia kipato zimekwama, usalama unazidi kuporomoka. Hata hivyo Claire Bourgeois mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini humo anasema wanachofanya sasa ni..
(Sauti ya Claire)
"Kutoa huduma za kuokoa maisha kwa wakimbizi wa ndani na jamii, na pili kuhakikisha walioathiriwa na mzozo wanalindwa hususan makundi yaliyo hatarini. Ndio maana tunazingatia mambo hayo mawili na kujikita katika kujenga uwezo kwa jamii zilizoathirika ziweze kustahimili na ndio maana tunataka wadau wa maendeleo wajumuike kwani hatimaye tunataka jamii irejee nyumbani na kuendelea na maisha yao Jamhuri ya Afrika ya Kati."
Ombi jipya la fedha kwa usaidizi ni dola Milioni 551 na kiasi kilichopatikana hadi sasa ni asilimia 30 pekee.

No comments: