Saturday 31 May 2014

Wabunge watuhumiana wizi

Sendeka: Muhongo, Maswi weziWABUNGE jana waligeuza Ukumbi wa Bunge sehemu ya mnyukano baada ya baadhi yao kushambuliana, huku wakituhumiana kwa wizi na wamehongwa na uongozi wa Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), jana waliwasha moto na kuibana serikali kutaka iunde Tume Maalumu kuchunguza kashfa ya ufisadi wa zaidi ya sh bilioni 200 zilizohifadhiwa kwenye akaunti ya Escrow ndani ya Benki Kuu (BoT).
Mbali ya kutaka Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza ufisadi huo, wabunge hao kwa nyakati tofauti walitaka serikali ichunguze kifo cha aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa, kwani wakati fedha hizo zinakwapuliwa, waziri huyo alikuwa Afrika Kusini akiugua na alishakata kauli.
Msimamo wa wabunge hao, uliungwa mkono na Mbunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka, ambaye alilitaka Bunge kuunda Kamati Teule kubaini ukweli wa kashfa hiyo.
Wabunge kwa nyakati tofauti waliwasha moto huo jana bungeni wakati wa mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa Fedha 2014/2015.
Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo, Mnyika, alisema kuwa wezi wa fedha za Escrow wako ndani ya Bunge hilo na maelezo yoyote kuwa  taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ifanye uchunguzi haitaungwa mkono na kambi ya upinzani kutokana na historia yake.
Huku akiungwa mkono na wabunge wote wa kambi ya upinzani, alisema Takukuru iliwahi kutumika kusafisha sakata la Richmond, hivyo hawana imani kama inaweza kuja na matokeo ya uchunguzi sahihi ya kashfa hiyo.
Alisema Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa (CAG), nayo ilihusika kumsafisha aliyekuwa Katibu Mkuu David Jairo, katika kashfa ya kugawa fedha kwa wabunge ili waiunge mkono na kupitisha Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Akaunti hii ilifunguliwa ili fedha ambazo Tanesco ilipaswa kuilipa IPTL kwa ajili ya tozo za uwekezaji ‘Capacity Charge’ ziwekwe hadi pale mgogoro huo utakapomalizika.
Mnyika, alisema kwa mujibu wa taarifa ya Gavana wa Benki Kuu, Benno Ndullu, aliyotoa katika kikao cha Kamati ya Uchumi ya Bunge kilichofanyika Bagamoyo, alikiri kuwa alibanwa na viongozi wa juu kiasi cha kushindwa kufurukuta.
Alisisitiza kuwa kauli za viongozi waandamizi wa serikali na Shirika la Umeme nchini kwa nyakati tofauti  kuhusu sakata hilo, zimezidisha utata na kuchochea dhamira ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutaka iundwe Kamati Teule ya Bunge kuchunguza.
Mnyika alihitimisha hoja yake kwa kukumbusha kwa mujibu wa Mtume Muhamad (SAW) aliyesema kuwa mnafiki ni mtu mwenye nyuso mbili, ndani yake na nje yake ni tofauti na alama zake ni tatu: akizungumza husema uongo, akiahidi hatimizi na akiaminika hufanya hiyana.
“Mheshimiwa Spika, unafiki uachwe kwenye mjadala wa mwaka huu tuweze kuishauri na kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi kwa kuzingatia maoni nitakayowasilisha.
“Mosi, spika aruhusu kabla ya mjadala huu kuendelea ziwekwe mezani nakala ya ripoti zote za kamati za uchunguzi kwenye sekta ya nishati na madini zilizoundwa na matokeo yake kutowasilishwa bungeni mpaka sasa.
“Pili, Wizara ya Nishati na Madini itakiwe kabla ya mjadala huu kuwasilisha kabrasha la majibu ya michango ya wabunge juu ya makadirio ya mwaka 2013/2014.
“Tatu, mara baada ya hoja hii kuamuliwa, naeleza kusudio la kuwasilisha hoja binafsi ya kutaka kuundwe kamati teule ya kuchunguza masuala tete na tata tuliyoyaeleza katika maoni haya ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
“Nne, Waziri Mkuu kwa mamlaka na madaraka yake kwa mujibu wa ibara ya 52 ya katiba ya nchi atakiwe katika mkutano huu wa Bunge kuelekeza serikali iwasilishe taarifa bungeni juu ya maazimio ya Bunge kufuatia uchunguzi uliofanyika kwa nyakati mbalimbali juu ya masuala yanayogusa sekta za nishati na madini kama tulivyoyaeleza,” alisema Mnyika.
Wakichangia hoja hiyo, Kafulila, alisema kama Waziri Muhongo na wenzake waliotuhumiwa katika kashfa hiyo ni wasafi, hawana sababu ya kuogopa kuundiwa Kamati Teule kuwachunguza.
Mbunge huyo ambaye ndiye aliyeibua kashfa hiyo bungeni, alisema ana ushahidi wa kutosha kuhusu kashfa hiyo na alipotakiwa na Spika Anne Makinda kuwasilisha ushahidi alionao, aliinua begi zima lenye nyaraka alizodai zinahusu namna wizi huo ulivyofanyika.
“Mheshimiwa Spika, hakuna dhambi mbaya duniani kama unafiki. Kama kweli Bunge hili linataka kujua ukweli, tuunde Kamati Teule, watu wametoa bilioni 200 kumpa Singasinga ambaye kule Kenya alikumbwa na skandal ya Goldenberg iliyoiangusha Serikali ya Kenya.
“Ushahidi ninao, lakini kila nikitaka kuuleta spika anakatakata kona,” alisema Kafulila.
Alisisitiza kuwa kuunda Kamati Teule kuchunguza jambo hilo sio kumsaka mchawi, hivyo Waziri Muhongo na wenzake hawana sababu ya kuwa na wasiwasi.
Kafulila, ambaye aliwasilisha ushahidi wa tuhuma hiyo, alisema kwa nchi makini, serikali pia ilitakiwa kufanya uchunguzi wa kifo cha Waziri Mgimwa, kwani wakati amezidiwa na ugonjwa nchini Afrika Kusini, huku nyuma fedha hizo zilichotwa kwenye akaunti hiyo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Simanjiro, Ole Sendeka, alipigilia msumari kutaka Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza ufisadi kwenye akaunti ya Escrow.
Sendeka ambaye ni mbunge pekee wa CCM mwenye msimamo unaofanana na kambi rasmi ya upinzani kwenye kashfa hiyo, alieleza jinsi fedha hizo zilivyohamishwa Benki Kuu kwenda Benki ya Standard Chartered na jinsi zilivyochotwa.
“Mheshimiwa Spika, kuna ushahidi wa namna vigogo walioshiriki kuchota fedha hizo, walihamisha dola milioni 5, (sawa na sh bilioni 8), siku nyingine watu wenye uhusiano na vigogo humu ndani walichota dola milioni 2, sawa na bilioni tatu), mara tano kwenye mifuko ya rambo na kusafirisha kinyume cha sheria ya kutakatisha fedha,” alisema Sendeka.
Huku wabunge wa CCM wakimshangaa, Sendeka kwa kujiamini zaidi alisema atawashangaa sana wabunge wa CCM watakaopinga kuundwa kwa tume hiyo ili kujua ukweli.
Jioni, Sendeka alisema ana ushahidi wa wezi wa Tanzania ambao badala ya kuwajibishwa wamekuwa wakipandishwa vyeo na wengine wamo ndani ya Bunge akiwemo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi.
“Ninao ushahidi hapa unaonyesha fedha zilizochotwa Tanesco, wizara, BoT na hata nikipigwa risasi nitaendelea kushikilia msimamo huo… nitakupa  ushahidi huo,” alisema.
Mnyika awasilisha ushahidi
Baada ya kutakiwa na spika kuwasilisha ushahidi mezani, Mnyika aliwasilisha nyaraka mbalimbali kuthibitisha kashfa hiyo ya akaunti ya Escrow.
Utoaji wa fedha za Escrow
Fedha za Escrow zilizotokana na malipo ya ‘capacity charges’, zilikuwa katika makundi mawili; moja ni fedha za Kitanzania na za dola za Marekani.
Kufikia Novemba 25, 2013, salio katika dola za Marekani, pamoja na faida lilikuwa ni dola 22,198,544.60, wakati salio katika fedha za Kitanzania lilikuwa ni sh 161,389,686,585.34, likijumuisha na faida katika uwekezaji ambayo ilikuwa sh 5,297,550,682.04.
Ulipaji wa fedha za Escrow kwa IPTL
Kutokana na maelekezo ya IPTL, Novemba 28, 2013 fedha taslimu, dola za Marekani 22,198,544.60 na shilingi 8,020,522,330.37 zililipwa katika akaunti iliyotolewa na IPTL.
Desemba 5, 2013 BoT ilihamisha Hati Fungani (Treasury Bond) yenye thamani ya sh  153,369,164,254.97 kwenda IPTL na kuhitimisha jukumu la BoT la kuwa wakala wa Escrow.
Desemba 19,  2013, BoT iliiomba Wizara ya Fedha kufunga rasmi akaunti ya Escrow kwa vile madhumuni ya kufunguliwa kwake yalifika mwisho.
Malipo ya Tanesco kwa IPTL
Wakati wa kufunga akaunti ya Escrow Desemba, 2013 Tanesco ilikuwa ikidaiwa na IPTL  dola za Marekani milioni 79.05 sawa na shilingi bilioni 125.04 zilizotokana na ununuzi wa umeme (Capacity Charge) ambazo hazijalipwa.

No comments: