Wednesday 4 June 2014

Lampard akaribia kutua Man City

Frank Lampard

 
NI kama hadithi, lakini wala haiwezi kushangaza sana kumwona kiungo, Frank Lampard, akikaribia kuvaa jezi ya Manchester City licha ya awali kuahidi kutovaa jezi ya timu nyingine yoyote zaidi ya Chelsea.
Habari kutoka England zinadai kwamba matajiri wa Manchester City ambao wamemnunua Lampard akachezee timu yao ya New York City ya Marekani, wanataka aichezee City kwa mkataba wa muda mfupi.
Mkataba wa Lampard Stamford Bridge umemalizika mwezi huu na yupo huru kujiunga na klabu yoyote anayoipenda baada ya Chelsea kuamua kutomwongezea mkataba mwingine kama ilivyo kwa Ashley Cole.
Ligi Kuu Marekani itaanza Machi mwakani na Manchester City wanataka Lampard asaini mkataba wa miezi sita kwa ajili ya kuichezea timu yao ya Etihad mpaka wakati huo.
Wiki tatu zilizopita, Lampard, ambaye atatimiza umri wa miaka 36 mwezi huu, alidai kwamba kamwe asingeweza kuvaa jezi ya timu nyingine na kucheza mechi dhidi ya Chelsea, lakini matajiri wa City wana matumaini kwamba Lampard atabadili mawazo kwa ajili ya kuongeza wachezaji Waingereza.
Wachezaji watano raia wa Uingereza; Micah Richards, Jack Rodwell, Gareth Barry, Scott Sinclair na Joleon Lescott, wote wanatazamiwa kuondoka katika dirisha hili na Manchester City iko hatarini kupoteza msingi wake wa wachezaji wa taifa hilo.
Lampard, ambaye juzi Jumapili alipaa na kikosi cha England kwenda Miami kwa ajili ya kujiandaa na fainali za Kombe la Dunia huku akiwa kama kocha msaidizi, ataungana na mshambuliaji wa Atletico Madrid, David Villa katika klabu ya New York City.

No comments: