Tuesday 10 June 2014

Wabunge wapinga vyakula kwa madai vinawanenepesha zaidi

Bi Zukile Luyenge
Wabunge wa Afrika Kusini wamelalamika juu ya chakula kinachopikwa katika mkahawa ulio katika majengo ya bunge wakisema kuwa kinawafanya kunenepa kupita kiasi.
Wabunge hao wamelalamika juma hili kwamba wengi wao huingia katika bunge hilo wakiwa wakonde na wadogo lakini wanaishia kunona kwa sababu ya vyakula visivyokuwa na afya vinavyopatikana katika mkahawa wa bunge.
Wakati wa warsha ya utambulisho juma hili, wabunge walilaani vyakula vya bunge, wakisema ndio sababu ya kunenepa kwao kwa mujibu wa jarida la kwenye mtandao la 'The Times live.'
''Sisi wabunge huingia katika bunge hili tukiwa na umbo nzuri wadogo na wa kupendeza, lakini muhula wetu unapokwisha , tutakuwa wanene kupindukia,'' alisema mbunge mmoja wa chama cha ANC ,Sheila Sithole.
Mbunge mwenzake Zukile Luyenge anakubaliana na kauli hiyo: ''Kila chakula kinachouzwa hapa kina mafuta mengi na proteni nyingi.''
Wanasiasa wanapofanya mikutano yao wakati wa mchana hulazimika kula Sambusa, Sausage au nyama ya Kondoo kati ya vyakula vingine vya mafuta vinavyouzwa kwenye mkahawa huo.
Wabunge wanasema mkahawa huo unauza Sambusa, Sausage na nyama ya aina aina
Chakula hicho kinanenepesha sana kiasi cha mbunge mmoja kuanza kukisusia na kuanza kula chakula chenye afya nje ya bunge.
Mnamo mwaka 2012, waziri wa afya nchini humo Aaron Motsoaledi, alianza kunenepa sana kwa kubugia chakula hicho ingawa alinukuliwa akisema , ''tatizo na kazi yao ni kwamba kuna chakula kila mahali.''
Hata hivyo mmoja wa wabunge hao anawashauri wenzake kuanza kufanya mazoezi ili kupunguza uzito.
Bi Sheila Sithole alisema, “Tulichogundua kuhusu vyakula vya hapa bungeni ni kwamba kila chakula kina mafuta na protini kwa wingi. Kwa kawaida, hufai kula mafuta mengi na Protini kwa wakati mmoja.”
“Kuna vyakula mbalimbali lakini vina mafuta, ikiwemo Samaki. Afadhali kula nyama kila wakati kuliko kula Samaki iliyopikiwa hapa bungeni,” alisema mbunge huyo.
Sithole amewataka wabunge kufanya mazoezi katika jumba la kufanyia mazoezi lililoko katika majengo ya bunge, kama anavyofanya mwenyewe iwapo watataka kuepuka unene.

No comments: