Monday 14 July 2014

Balali alikataa maiti yake isionyeshwa hadarani wala asizikwe Tanzania


“Ni kweli nilishiriki kwenye maziko kwa sababu mimi kama Balozi wa Tanzania wakati huo ndiye nilikuwa mwakilishi wa Serikali pale Washington, lakini jambo la pili ni kwamba binafsi nilimfahamu Ballali kwa muda mrefu, kwa hiyo hata kama nisingekuwa balozi lazima ningekwenda kuzika tu.” Balozi Ombeni Sefue.

Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania BOT), Marehemu Daudi Ballali aliacha wasia unaotaka maiti yake isionyeshwe hadharani atakapofariki dunia na wala maiti yake isiletwe Tanzania kwa ajili ya maziko.
Ballali aliyefariki Mei 16, 2008 na kuzikwa Mei 23 mwaka huohuo katika makaburi ya Gate of Heaven, eneo la Silver Spring, Maryland nchini Marekani alifahamu kuhusu kifo chake wiki mbili kabla, baada ya matibabu kushindikana.
Mwandishi wa Mwananchi aliyekuwa nchini Marekani kwa siku kumi kufuatilia suala hilo, alibaini kuwa kiongozi huyo alilazwa mara ya pili katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha George Washington, April 2008 na alirejea nyumbani kwake, Washington DC wiki mbili kabla ya kukutwa na mauti.
Habari kutoka ndani ya familia yake zinasema baada ya madaktari kushindwa kumtibu walimwambia kwamba asingeweza kuishi kwa zaidi ya wiki mbili, hivyo walimshauri ahamie kwenye ‘hospice’ ambayo ni nyumba maalumu ya kusubiri kifo kwa watu ambao magonjwa yao yameshindikana.
Hospice hutumika kwa ajili ya kuwaweka wagonjwa wanaohitaji faraja hasa kutoka na maumivu makali chini ya uangalizi wa washauri na wauguzi kwa lengo la kuwaongezea wagonjwa husika siku za kuishi.
Baadhi ya hospice hutoa huduma za kiroho, kijamii na kifedha na wakati mwingine huduma hizo hutolewa kwa wagonjwa ambao wanaugulia nyumbani. Hata hivyo, gazeti hili lilidokezwa kwamba Ballali alikataa kwenda kwenye nyumba hiyo na badala yake kutaka apelekwe nyumbani kwake.
“Alikataa kwenda kwenye hospice, aliwaambia madaktari kwamba yeye hawezi kwenda huko ijapokuwa kuna huduma nzuri na uangalizi wa nesi (muuguzi). Aliwaambia kwamba nitakwenda kufia nyumbani kwangu maana nina nyumbani kwangu,” kilisema chanzo chetu na kuongeza:
“Aliporejeshwa nyumbani, alikuwa anazungumza kama kawaida lakini kadri siku zilivyosogea hali ilikuwa ikibadilika na kama sikosei siku mbili au tatu za mwisho (za uhai wake) alikuwa anajitambua lakini alikata kauli, hakuwa akizungumza chochote”.
Uchunguzi wetu umebaini kuwa katika siku hizo za mwisho za uhai wake, Ballali aliacha maelekezo kwamba pindi atakapofariki dunia, mwili wake usiwekwe hadharani kwa maana ya kutazamwa na watu nje ya familia wala kusafirishwa kuja Tanzania kwa ajili ya maziko.
“He said, he doesn’t like to be turned into a laughing staff (alisema asingependa kugeuzwa kichekesho), sababu watu wasingekuja kutoa heshima za mwisho, bali wangekuja kumdhihaki kuangalia Ballali aliyetuhumiwa kwa ufisadi wa EPA na siyo Gavana,” kilisema chanzo hicho.
Kifo, mazishi yake
Habari kutoka ndani ya familia yake zinasema Ballali alifariki Mei 16, 2008 saa 8:00 mchana saa za Marekani, sawa na saa 03:00 za Tanzania akiwa nyumbani kwake, Maryland.
Baada ya kifo chake, mwili wake ulihifadhiwa kwenye nyumba ya maiti iitwayo Vol Funeral Home iliyopo Washington DC kwa siku nne na siku ya tano Mei 23 uliondolewa na kupelekwa Kanisani kwa ajili ya Ibada kisha kupelekwa makaburini kwa ajili ya maziko.
Siku hiyo ya Mei 23 saa nne asubuhi, familia ya Ballali ikiongozwa na mjane wake Anna Muganda pamoja na watoto wake wawili, mtalaka wake na wanafamilia wengine, walikwenda Vol Funeral Home ambako walitoa heshima za mwisho kwa marehemu.
“Katika tukio hilo familia ilikubaliana kwamba matakwa ya marehemu yaheshimiwe, kwa hiyo hakuna aliyeruhusiwa kupiga picha zozote. Kwa hiyo ni ndugu tu wa familia walioruhusiwa kuona mwili wa Ballali, baadaye tulifunga casket (jeneza) na tukaondoka kwenda Kanisani,”kilisema chanzo chetu nchini Marekani.
Kauli hiyo inaungwa mkono na maelezo yaliyotolewa kwa gazeti hili Agosti 25, 2013 na dada wa Marehemu Ballali, Margaret Mpango kwamba shughuli za kuaga mwili wa marehemu, ibada na baadaye maziko vilikuwa ni kwa ajili ya familia pekee.
Akizungumza na Mwandishi wa Mwananchi, nyumbani kwake mjini Kigoma, Margaret Mpango aliweka bayana kwamba: “Familia isingeweza kuruhusu watu wengine kushiriki, haikuwa na maana yoyote kwani tayari kulikuwa na maneno mengi yanayomhusu”.
Dada huyo anayezaliwa tumbo moja na Marehemu Ballali ni mke wa Askofu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Kasulu, Kigoma, Dk. Gerald Mpango ambaye alikuwa miongoni mwa walioongoza Ibada ya maziko ya Ballali.
Margaret alilithibitishia gazeti hili kwamba mumewe (Dk. Mpango), alishirikiana na mapadre wa Kanisa la Mtakatifu Stephen, Washington D.C. kuongoza ibada ya mwisho ya Ballali ambaye siku hiyohiyo alizikwa katika makaburi yanayomilikiwa na Kanisa Katoliki ya Gate of Heaven.
Alisema miongoni mwa waliohudhuria mazishi hayo ni aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani wakati huo, Balozi Ombeni Sefue, ambaye hivi sasa ni Katibu Mkuu Kiongozi.
Kauli ya Sefue
Jana Balozi Sefue akizungumza na Mwandishi wa Mwananchi, alithibitisha kwamba kweli alishiriki kwenye Ibada ya kumuaga Ballali na baadaye kwenye maziko ya Gavana huyo katika makaburi ya Gate of Heaven
 
“Ni kweli nilishiriki kwenye maziko kwa sababu mimi kama Balozi wa Tanzania wakati huo ndiye nilikuwa mwakilishi wa Serikali pale Washington, lakini jambo la pili ni kwamba binafsi nilimfahamu Ballali kwa muda mrefu, kwa hiyo hata kama nisingekuwa balozi lazima ningekwenda kuzika tu,” alisema Balozi huyo.
Picha zake zasakwa
Taarifa zaidi ambazo gazeti hili lilizipata Washington DC, zinasema kulikuwa na jitihada za kutaka kupiga picha mwili wa marehemu wakati wa kutoa heshima za mwisho, lakini zilikwama baada ya ndugu wa marehemu kuzima jaribio hilo.
“Mmoja wa waliokuwapo kwenye msiba baada sisi kumaliza kutoa heshima za mwisho alitaka kupiga picha kwa madai kwamba anataka kubaki na sura ya ndugu yetu, lakini tulikataa na kumwambia kwamba tulishakubaliana kutofanya hivyo kwa heshima ya marehemu,” kilieleza chanzo chetu na kuongeza:
“Baadaye tulipata taarifa kwamba wapo watu tena kutoka Tanzania ambao walikuwa wakihitaji picha hiyo kwa udi na uvumba na walikuwa wameahidi kuinunua kwa Dola za Marekani 35,000”. Kiasi hicho ni sawa na Sh57.7 milioni kwa viwango vya sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni wastani wa Sh1650 kwa dola moja.
Safari ya Marekani
Safari ya Mwandishi wa Mwananchi nchini Marekani ilianza Alhamisi Juni 26, 2014 hadi Jumapili, Julai 6. Mwandishi wa habari hizi aliligundua kaburi hilo baada ya kwenda makaburi ya Gate of Heaven kwa siku tatu mfululizo.
Siku ya kwanza, mwenyeji wa mwandishi ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sasa alimfikisha katika makaburi hayo, lakini kaburi la Ballali halikuonekana na hata mwandishi alipokwenda siku ya pili peke yake, kaburi hilo pia halikuonekana kwa kutokana na ukubwa wa eneo hilo.
Siku ya tatu, Mwandishi wa Mwananchi alilazimika kuomba msaada wa Ofisi ya Makaburi ya Gate of Heaven, ambayo ilimsaidia kuonyesha eneo lilipo kaburi hilo, hivyo kuwezesha kupata picha zake.
Kaburi lake liko katika msitari wa mwisho kabisa na Ukanda wa Kijani wa miti iliyozunguka makaburi ya Gate of Heaven, likiwa limeandikwa jina la kiongozi huyo, pamoja na maneno ya Kiingereza yanayosomeka “When the heart weep for what it has lost, the soul rejoices for what it has found”.Maana ya maneno hayo ni kwamba, “Wakati moyo ukiomboleza kwa kile kilichopotea, roho hufurahi kwa kile kilichopatikana”. Kaburi hili limezungukwa na makaburi mengine kadhaa ambayo si ya Watanzania, kwani kwa haraka kutokana na mazingira yalivyokuwa, Mwandishi wa Mwananchi hakuweza kuona kaburi jingine lenye majina yenye asili au kuwa na mwelekeo wa asili ya Tanzania.

No comments: