Monday 21 July 2014

Chadema yashikilia msimamo wa kutoshiriki Bunge la Katiba

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salam jana, kuhusu maazimio ya Kamati Kuu ya Chama hicho, iliyokutana kwa siku mbili Dar es Salaam, Kushoto ni Katibu Mkuu wa chama hicho Dk. Wilbrod Slaa.


Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka katika chama chake hawatashiriki katika Bunge hilo linalotarajiwa kuendelea mwezi ujao.
Aidha, amesema Chadema haitashiriki katika kikao cha Julai 24 kilichoitishwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samwel Sitta akisema hicho ni sehemu ya Bunge hilo ambalo wajumbe wake na wenzao wanaounda Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa) walilisusia.
Akisoma tamko la Kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mbowe alisema iwapo Bunge hilo litapitisha Rasimu ya Katiba Mpya isiyotokana na maoni ya wananchi, chama hicho kikiwa sehemu ya Ukawa, kitafanya kampeni nchi nzima kuwashawishi wananchi kuikataa wakati wa upigaji wa kura ya maoni.
Alisema kuliko kupata Katiba Mpya ambayo ni mbovu ni bora mchakato wa kuipata uchelewe ili Ukawa waendelee kupigania Katiba bora itakayopatikana kutokana na maoni ya wananchi na siyo maoni ya CCM.
Wakati Mbowe akieleza hayo, CCM Zanzibar kimeibuka na kutaka Ukawa kuacha visingizio na badala yake waungane na wabunge wengine kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba bila ya kutoa masharti.
Katibu Mwenezi wa CCM Zanzibar, Waride Bakari Jabu alisema hayo alipokuwa akizungumza na wajumbe wa nyumba kumi, mashina, matawi, wadi na jimbo huko Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema siyo busara kwa wabunge wa Ukawa kutoa visingizio visivyo na mashiko na kutozingatia masilahi ya umma na tija ya kupatikana kwa Katiba Mpya ijayo mwaka 2015.
Mambo manne
Mbowe alitaja mambo manne kabla ya Ukawa kurejea bungeni akisema ni kuendeleza mazungumzo na Rais Kikwete kwani ndiye msimamizi mkuu wa mchakato wa Katiba.
“Kamati Kuu imebariki kuendelea kwa mazungumzo kati ya Rais Kikwete na Ukawa, pia upande wa Serikali kuhusu namna ya kunasua mchakato huu ndani ya Bunge Maalumu. Kikao cha Sitta ni sehemu ya Bunge la Katiba, sisi kama Chadema na Ukawa pia hatutashiriki kikao hicho kwa sababu tunaamini kitakachojadiliwa hakitapishana na yaliyotokea bungeni.”
Julai 8 mwaka huu, Sitta aliitisha kikao cha wajumbe 27 wa kamati ya mashauriano wakiwamo maaskofu wawili ili kuondoa mpasuko kati ya Ukawa na wajumbe wengine.
Alisema licha ya kuwapo mazungumzo ya kuwataka Ukawa kurejea bungeni, CCM kimekuwa kikitumia mwanya huo ili wakirejea kiendeleze mkakati wake wa kubadili kila jambo katika rasimu hiyo
“Kesho (leo) tutakutana na CCM ila siwezi kukwambia ni wapi. Tunaamini mazungumzo na Rais Kikwete ndiyo yanaweza kunusuru mchakato huu,” alisema Mbowe.
Alisema jambo la pili, wajumbe wa Ukawa kutoka Chadema watarejea kwenye vikao vya Bunge hilo endapo mamlaka ya Bunge la Katiba itafafanuliwa kuwa ni kuboresha na si kuibomoa au kuifuta misingi mikuu ya rasimu hiyo.
“Tatu, wajumbe wa Ukawa kutoka Chadema watarudi bungeni iwapo ufafanuzi uliotajwa katika sura ya pili, utahusisha marekebisho ya Kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba” alisema Mbowe.
Akitaja sababu ya nne, Mbowe alisema wajumbe kutoka chama hicho hawatarejea bungeni hadi ufafanuzi wa mamlaka ya Bunge hilo uliotajwa katika sura ya 2 na 3 utakapofanyika.
“Endapo kwa sababu yoyote ile Bunge Maalumu litavunjwa kabla ya kupitishwa Rasimu ya Katiba. Chadema kama sehemu ya Ukawa itafanya mapambano ya kupata Katiba Mpya ya kidemokrasia kuwa sehemu kuu ya kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015,” alisema Mbowe.
Waliojiengua Chadema
Akizungumzia viongozi wa chama hicho waliojiuzulu nyadhifa zao mkoani Kigoma na Tabora, Mbowe alisema hao ni mamluki na wameshindwa kukifanya chama hicho kipate wabunge wengi katika mikoa hiyo... “Kama ambavyo mawakala wa CCM wa miaka ya nyuma hawakuathiri kukua kwa Chadema, wasaliti na mawakala wa CCM wa sasa na wasaliti na mawakala watarajiwa hawataweza kuathiri kukua na kujiimarisha kwa chama chetu.”
Viongozi wote wa Chadema Mkoa wa Kigoma walijivua uanachama wa chama hicho juzi. Hao ni Mwenyekiti, Jafari Ramadhani Kasisiko, katibu wake; Msafiri Hussein Wamalwa Malunga na Katibu wa Baraza la Wanawake, Masoud Simba. Pia Katibu wa Chadema Mkoa wa Tabora, Athumani Balozi na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la chama hicho wa mkoa, Hussein Kundecha nao walijiuzulu.

No comments: