Saturday 19 July 2014

Dr silaa adai Chadema ilishinda Uchaguzi 2010

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (Kulia) akiteta jambo na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willbrod Slaa wakati wa kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika jana Dar es Salaam
 

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kuwa kinaamini kilishinda uchaguzi wa rais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 chini ya mfumo wa vyama vingi.
Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willbrod Slaa, ambaye pia alikuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho kwenye uchaguzi huo, alibainisha hayo hivi karibuni wakati wa mahojiano maalumu na waandishi wa gazeti hili.
Dk Slaa alisema kuwa ana uhakika kuwa chama chake kilipata kura nyingi zaidi za urais, tofauti na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Mrisho Kikwete aliyetangazwa mshindi.
“…Baada ya uchaguzi wa mwaka 2010, tulikataa kumtambua Rais Kikwete, ingawa wakati ule hatukujua kwa uhakika kama tulishinda. Kadiri nilivyozunguka, ndiyo kadiri tulivyoanza kuamini kwamba tulishinda,” alisema Dk Slaa.
Alisema kuwa takwimu walizonazo zinaiaminisha Chadema kwamba ilishinda Uchaguzi Mkuu wa urais mwaka 2010.
“Sababu, unafika kwenye jimbo wanakusomea kura ulizopata katika uchaguzi ule wakizilinganisha na alizozipata Kikwete na Profesa Ibrahim Lipumba… wanasema Dokta hapa ulimshinda… kwa kura 20,000, pale ulimshinda kwa kura 15,000 pale ulimshinda kwa kura…,” alifafanua na kusisitiza:
“Sasa ndiyo, tuna uhakika kama tulishinda na ndiyo maana Kikwete hajawahi kwenda kwa wananchi kushukuru kwa kumchagua, tofauti na tabia yake. Anachofanya sasa ni kwenda kuzindua miradi.”
Hata hivyo, Dk Slaa alisema hawakuweza kuendelea na madai yoyote kwa sababu kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya nchi, mshindi wa urais akishatangazwa hairuhusiwi kupinga kwa namna yoyote hata mahakamani, akieleza kuwa hiyo pia ndiyo sababu ya kuhitaji Katiba Mpya.
Tume ya uchaguzi na CCM
Alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Mstaafu Damian Lubuva alisema anasubiri kwanza kusoma kwenye vyombo vya habari alichokisena Dk Slaa ndiyo ataweza kuzungumzia suala hilo.
“Kwa kuwa wewe ndiyo umeniambia Dk Slaa amesema hivyo, ngoja nione kwanza halafu tume itatoa maelezo,” alisema Jaji Lubuva.
Alipopigiwa simu Makamu Mwenyekiti wa CCM- Bara, Philip Mangula ili atoe ufafanuzi kuhusu suala hilo, alimsikiliza mwandishi wetu, kisha akasema yupo katika kikao na kukata simu
Wizi wa kura
Alipoulizwa kama wanaelewa kura zinavyoibwa kutokana na malalamiko ya mara kwa mara ya Chadema na vyama vingine vya upinzani, Dk Slaa alisema:
“Watu wengi wanafikiri huo ni wimbo tu wa kila siku, sasa kama tunaibiwa tunyamaze? Tuseme uongo kama hatukuibiwa kura…? Hakuna uwanja sawa katika uchaguzi.
“Uchaguzi kimsingi ni uwanja wa mpira. Umeshaona kama katika uwanja wa mpira upande mmoja kuna kichuguu na kinaachwa pale? Kinaondolewa. Kilichokosekana nchi hii ni dhamira ya kuondoa vichuguu katikati ya kiwanja cha mpira; usipoondoa hivyo vichuguu hutapata uchaguzi wa haki hata siku moja.”
“Kumbuka Arumeru tulitangaza, tukasema tumegundua vituo hewa 55 vyenye jumla ya wapigakura 20,000, tulitangaza. Bahati nzuri pale tuliweza kusimamia na mnakumbuka pale tulivyotukanana na ofisa wa polisi ambaye leo ni DCI, unaweza kumpigia simu Mwigulu Nchemba akueleze jinsi tulivyotunishiana misuli… tukafanikiwa pale kuokoa kura 20,000,”alisema.
Aliongeza: “Kalenga tulipiga kelele mwanzoni kabisa kuhusu kuwapo majina mapya kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura, kama daftari liliboreshwa… yaliingiaje kwenye daftari hili la 2010. Ndiyo maana hatuna imani na Tume ya Uchaguzi….”
Alibainisha: “Mimi nina uzoefu wa kesi za uchaguzi katika ushindi wangu mara tatu Jimbo la Karatu hakuna hata mara moja ambayo sijapelekwa mahakamani.
“Mara ya mwisho niliponea chupuchupu, ndiyo akili ikafunguka. Hukumu ilitolewa niwafungulie CCM kesi ya kughushi. “Kwa sababu mahakama ilikuta kura zaidi ya 5,000 kupitia fomu namba 21b (result form) siyo sandukuni ndipo walipoibia, lakini kwenye matangazo ya awali nilishinda kwa kura 1,060, wamekwenda mahakamani wakasema wamenishinda kwa kura 177.
“Kwa miezi mitatu niliangalia bila kugundua, nikipiga hesabu naona ni kweli, kumbe walitengeneza vituo hewa na katika vituo vya kujumlisha kura na kuvipa namba kama iliyopo kwenye fomu halali za matokeo na kujaza kura za wizi. Waliipa CCM kura 300, Dk Slaa kura 20, za kwao zilipanda zangu zilishuka, makahama imesema kazi hiyo haikufanywa kijijini bali na wataalamu, ndiyo maana tunataka Tume Huru ya Uchaguzi ili kuwa na uwanja sawa katika uchaguzi.”
Wingi wa wanachama CCM/Chadema
Kuhusu wingi wa wanachama wa Chadema na CCM, Dk Slaa alisema: “Kwa taarifa yako nina taarifa ya mkaguzi aliyewauliza CCM orodha ya wanachama wake ikashindwa kutoa. Kama hawana orodha ya wanachama, hiyo milioni sita wanaitoa wapi? Uongo, ‘nawachalenji’ watoe hadharani….”
“Ushahidi wa pili, kujua kama una wanachama ni uhai wa wanachama. Taarifa ya CCM ya 2010 inaonyesha kwamba walikuwa wanapata kutoka kwa wanachama wao Sh9 bilioni za kadi kama ada, zimeshuka hadi Sh2 bilioni, utahesabu ni wangapi hao. Wasitudanganye…, tuna vyanzo vingi vya kupata taarifa.

Mimi sitakupa leo nina wanachama wangapi kwa sababu tunafunga kompyuta kwenye kila kanda, jimbo na kata, tumeanzisha ‘data base’ baada ya kukamilika nitakwambia tuna wanachama wangapi,” alisema na kuongeza:
“Uongo wa CCM usikudanganye kwamba nguvu yao ni wanachama, kama nguvu yao ni wanachama, uchaguzi haupigiwi kura na wanachama, kura zinapigwa na wapigakura, wananchi wanaotaka huduma kwa sababu wanalipa kodi.
Wanapiga kura ili wapate kiongozi ili asimamia kodi zao, waondokane na maisha magumu, wapate huduma za afya na elimu bora...”

No comments: