Sunday 20 July 2014

Israel yaanza operesheni ya ardhini Gaza

Image
Wakati mashambulizi hayo ya Israel kwa Gaza yakiingia siku yake ya 11 kwa jeshi la nchi hiyo kuushambulia ukanda huo wa mwambao kwa njia ya anga na majini halikadhalika kwa kutumia vifaru viliyokusanywa mpakani, idadi ya maafa ya Wapalestina imeongezeka na kupindukia 260.
Raia wamekuwa wakikimbia maeneo yenye kupakana na mpaka wa Israel ambapo zaidi ya watu 30,000 wametafuta higadhi kwenye vituo vya Umoja wa Mataifa. Miongoni mwa waliouwawa wakati wa mashambulizi hayo ya usiku ni mwanajeshi mmoja wa Israel na mtoto mchanga wa miezi sita.
Taifa hilo la Kiyahudi limesema linaendelea na operesheni kuangamiza mitandao ya mahandaki iliyojaa Gaza inayotumiwa na wanamgambo wa Kipalestina kutengenezea maroketi na kuishambulia Israel. Katika hatua isio ya kawaida Israel ilitangaza operesheni yake hiyo ya ardhini kabla hata ya kuanza.
Njia pekee kuangamiza mahandaki
Waatalamu wanasema operesheni hiyo ya ardhini ni njia pekee ya kufikia maeneo yanayokusudia ambao hayawezi kufikiwa kwa njia ya anga kama vile mtandao huo wa mahandaki. Kabla ya kuanza operesheni hiyo jana usiku, jeshi lilisema lilizima uvamizi wa chini ya ardhi ambapo wanamgambo 13 wa Gaza waliweza kujipenyeza kusini mwa Israel kabla ya kugunduliwa na wanajeshi. Ndege za kivita zilimuuwa mmoja wao na waliobakia wamerudi tena kwenye mahandaki walikotokea.
Lakini maroketi ya wanamgambo yameendelea kuvurumishwa Israel wakati wa usiku ambapo tisa yameanguka nchini humo na mengine tisa yamedunguliwa hewani.
Hamas kundi lenye kutawala Gaza limesema operesheni hiyo ya Israel itashindwa. Mkuu wa Hamas aliyeko uhamishoni akizungumza kutoka Doha, Qatar, amesema kile ilichoshindwa kufanikisha Israel kwa mashambulizi yake ya anga na baharini haitoweza kufanikisha kwa mashambulizi ya ardhini.
Awali afisa mwandamizi wa Hamas, Osama Hamdan, amesema kundi hilo liko tayari kukabiliana na operesheni hiyo ya ardhini.
Umwagaji damu kuongezeka
Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Wapalestina ameonya kwamba operesheni hiyo ya Israel itakuja tu kusababisha kwa umwagaji damu mkubwa zaidi na kuzidi kukwamisha juhudi za kusitisha mapigano.
Uvamizi huo wa Israel unafuatia usitishaji wa mapigano wa muda mfupi kwa misingi ya kibinaadamu na wito wa kidiplomasia wa dharura kwamba Israel iongeze juhudi za kuepusha madhara kwa raia.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameitaka Israel kuweka lengo mahsusi la kupunguza maafa yanayowahusisha raia wasiokuwa na hatia katika mashambulizi yake dhidi ya Gaza.

No comments: