Wednesday 23 July 2014

Machafuko bado yaendelea Libya

Kuendelea machafuko nchini LibyaMachafuko nchini Libya si tu kwamba yamekuwa ni kitu cha kila siku, bali kadiri muda unavyopita, ndivyo machafuko hayo yanavyoongezeka. Habari zinasema kuwa, mapigano yanaendelea kwa siku kadhaa sasa karibu na Uwanja wa Ndege wa Tripoli na hii ni katika hali ambayo mji wa Benghazi nao unaendelea kushuhudia mauaji dhidi ya wanasiasa, maafisa wa kijeshi na raia wa kigeni. Tukio la karibuni kabisa huko Benghazi ni kuchinjwa na kukatwa kichwa kibarua mmoja raia wa Ufilipino. Habari nyingine zinasema kuwa, wawakilishi wawili kutoka miji ya Benghazi na Janzur katika Congress ya Taifa ya Libya (Bunge) wametekwa nyara na watu wenye silaha. Mauaji dhidi ya maafisa wa kijeshi wa Libya nayo yanaendelea mashariki mwa nchi hiyo. Hivi sasa hali ya Libya ni mbaya sana; na jambo hilo linaonekana katika miundo yote ya kisiasa, kiuchumi ya kijamii ya nchi hiyo. Katika upande wa kisiasa na licha ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi na kujulikana muundo wa Bunge la nchi hiyo, lakini hadi hivi sasa zoezi la kukabidhi madaraka kutoka Congress ya Taifa kwenda kwa bunge jipya halijafanyika. Sababu yake ni kuwa hali ya Libya haiiruhusu nchi hiyo kutangaza siku ya kufanyika kikao cha kwanza cha bunge hilo jipya. Katika upande wa masuala ya kijamii pia ni kwamba, hakuna umoja na mshikamano wowote wa kitaifa nchini Libya. Kila sehemu nchini humo imo mikononi mwa kabila au pote fulani la watu na kwamba ni viongozi wa kikabila ndio wanaoongoza baadhi ya maeneo ya Libya. Mfano wa wazi ni maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo ambayo yamejitangazia utawala wa ndani na kadiri siku zinavyopita ndivyo maeneo hayo yanavyozidi kutoka mikononi mwa serikali kuu kiasi kwamba maeneo hayo hata yameanza kuchimba mafuta bila ya idhini ya serikali ya Tripoli. Katika upande wa kiuchumi pia, maeneo mengi ya mafuta yako mikononi mwa viongozi wa kikabila. Jambo hilo limeathiri vibaya sekta ya usafirishaji nje mafuta nchini Libya na kupunguza mno pate la serikali kuu. Hali hiyo kusema kweli inaufanya mustakbali wa Libya kukumbwa na giza nene. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, si jambo lililo mbali kuiona Libya ikigawika vipande vipande. Hali ilivyo Libya inaonesha wazi kuwa, machafuko ya nchi hiyo yanachochewa na mikono ya nje. Wanaochochea machafuko hayo ni yale madola ambayo kwa muda mrefu yalikuwa yanaukodolea macho ya tamaa utajiri mkubwa wa mafuta na gesi wa nchi hiyo. Tunathubutu kusema kuwa, hali ya hivi sasa ya Libya ni jinamizi kwa wananchi wa nchi hiyo, lakini wakati huo huo ni ndoto nzuri ya usingizi mnono kwa dola la Marekani na madola mengine ya Magharibi.

No comments: