Wednesday 30 July 2014

Mwanamke ajinyonga huko Tabata

Mwanamke aliyefahamika kwa jina la Irene Ibrahim (22), mkazi wa Tabata Kisukuru manispaa ya Ilala, amefariki dunia baada ya kujinyonga.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alisema marehemu alikutwa kwenye shamba la Abdallah Mshindo akiwa amejinyonga kwa kutumia khanga aliyoitundika katika tawi la mti aina ya mjohoro.
Minangi alisema, tukio hilo lilitokea Julai 27 majira ya saa 1 usiku, ambako Irene alifika kwenye duka la Oliver Laurent akiwa amebeba pombe tatu aina ya viroba na dawa aina ya Mifupain nyingi mkononi huku akiwaeleza baadhi ya watu kuwa, atasafiri kwenda Amerika kisha kuingia chumbani kwake.
Alisema, baada ya kuingia chumbani kwake, hakuonekana tena mpaka walipoangalia chumbani kwake walikuta maganda ya viroba na dawa bila yeye kuwepo, ndipo alipokutwa akiwa amejinyonga shambani hapo.
Katika tukio jingine, mtu mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja amefariki dunia baada ya gari alilokuwa akiendesha kugonga mti.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Camillius Wambura, alisema ajali hiyo ilitokea Julai 28 majira ya saa 8 usiku eneo la Masaki Kata ya Msasani, Kinondoni barabara ya Kimweri iliyohusisha gari aina ya Toyota Rav 4 yenye namba za usajili T422 AXV iliyokuwa inaendeshwa na dereva anayekadiriwa kuwa na miaka kati ya 20-25.
Wambura aliongeza kuwa, gari hilo lilikuwa linatokea barabara ya Ally Hassan Mwinyi kwenda Coco Beach ndipo lilipoacha njia na kugonga mnazi uliyokuwa kandokando ya barabara  hiyo.

No comments: