Tuesday 29 July 2014

mwanamke jambazi sugu na wenzake watiwa mbaroni

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kukamata mtandao hatari wa majambazi kumi, mmoja akiwa ni mwanamke anayeshiriki kikamilifu wakati wa matukio ya ujambazi.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna (CP), Suleiman KovaAkizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna (CP), Suleiman Kova, alisema majambazi hao wamekamatwa katika msako mkali unaoendelea katika harakati za kuhakikisha maisha na mali za wakazi wa Dar es Salaam vinalindwa kikamilifu.
Kova alisema katika msako huo watuhumiwa walipekuliwa katika miili, makazi na maficho yao na wakakutwa na silaha tisa ambazo ni bunduki SMG namba 13975 ikiwa na risasi 11 na magazine mbili, SMG moja bila magazine na namba hazisomeki, bastola aina ya Luger yenye namba 5533K, bastola aina ya Browning yenye namba TZACR83494 S/No.7670 na risasi sita ndani ya magazine.
Alizitaja silaha nyingine kuwa ni shotgun pump action na risasi 55, Marck Iv iliyokatwa mtutu na kitako yenye magazine moja na risasi nne, bastola yenye namba A963858 Browning iliyokuwa na risasi moja, SMG ambayo iko kwa mtaalam wa uchunguzi wa silaha (Balistic), pamoja na shotgun TZ CAR 86192 ambayo ilitelekezwa baada ya msako.
Kova aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Maulidi Mbwate (23), mfanyabiashara mkazi wa Mbagala Charambe, Foibe Vicent (30), hana kazi mkazi wa Mbagala Kibondemaji, Vincent Kadogoo (30), mkazi wa Mbagala Kibondemaji, Said Mlisi (29), dereva wa bodaboda mkazi wa Gongo la Mboto na Hemed Zaga (22), dereva bodaboda mkazi wa Gongo la Mboto.
Wengine ni Mohamed Said (31), fundi kuunga vyuma mkazi wa Kigogo, Lucy Mwafongo (41), mama lishe mkazi wa Vingunguti Ukonga, Rajabu Ramadhani (22), mkazi wa Kariakoo, Deus Chilala (30), mgonga kokoto Kunduchi, mkazi wa Yombo Kilakala pamoja na Marietha Musa (18), mkazi wa Yombo Kilakala.
“Mwanamke pekee katika kundi hilo Foibe Vicent ameshiriki katika matukio ya uporaji wa kutumia silaha, mauaji na mengine mengi, yeye mwenyewe alikuwa akitumia bunduki aina ya SMG. Katika baadhi ya matukio, wananchi walioshuhudia wamekuwa wakitoa taarifa kwamba alikuwepo mwanamke aliyekuwa akifyatua risasi na hatimaye polisi walifanikiwa kumkamata akiwa na wenzake katika kundi hilo,” alisema Kova.

No comments: