Monday 28 July 2014

Shirikisho la soka la Tanzania ndio linalo wanyima ulaji wachezaji

Kwa muda mrefu sasa wapenzi, mashabiki na wadau wa soka wamekuwa wakisema umefika wakati wa kuondoka katika soka la ridhaa na kuingia soka la kulipwa.
Kauli hii ya kuondoka katika soka la ridhaa na kuingia soka la kulipwa imesemwa sana, lakini uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) umeshindwa kuifanyia kazi.
Allan Goshashi 
Nasema hivyo

kwa sababu sera ya maendeleo ya michezo ya Tanzania inasema vyama vya michezo vimo katika makundi matatu makubwa ambayo ni (a) vyama vya ridhaa vilivyosajiliwa na msajili wa vyama vya michezo na kujishirikisha na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), (b) Mashirikisho ya michezo ambayo yameundwa na taasisi mbalimbali ili kutoa burudani za kimichezo kwa wafanyakazi, kuwakutanisha wachezaji wao ili wafahamiane, pia kuwashindanisha katika michezo inayohusika na kupata mabingwa wao katika ngazi ya taifa, (c) Vyama vya michezo ya kulipwa ambavyo vimesajiliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Mwaka jana TFF ilifanya mabadiliko ya katiba yake na baada ya hapo iliipeleka BMT ili mabadiliko hayo yapate baraka za BMT hali iliyoonyesha TFF ni chama cha ridhaa kilichosajiliwa na msajili wa vyama vya michezo ya ridhaa.
Chama cha mchezo wa kulipwa nchini ni Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) ambacho kimesajiliwa Wizara ya Mambo ya Ndani.
Vipo vyama vingine vya ngumi ambavyo vimeingia zaidi kwenye biashara ya ngumi za kulipwa na vimesajiliwa kama makampuni kwa msajili wa makampuni katika Wizara ya Viwanda na Biashara, Vyama hivyo ni TPBO na PST.
TFF ina wanachama, kushindwa kwake kujisajili kama chama cha mchezo wa kulipwa ndiyo kunaposababisha hata wanachama wake kushindwa kuingia kwenye soka la kulipwa.
Wanachama wa TFF ni pamoja na klabu zote 14 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Nakumbuka kuna wakati katika klabu ya Yanga kulikuwa na wanachama wa klabu hiyo waliojulikana kwa jina la Yanga Kampuni waliokuwa wakitaka iendeshwe kama kampuni na wengine waliokuwa wakitaka iendelee kuendeshwa kiridhaa (Yanga-asili).
Wale waliokuwa wakitaka Yanga iendeshwe kama kampuni walishindwa kufikia lengo lao na hata leo wakitaka Yanga iendeshwe kama kampuni watashindwa kwa sababu Yanga ni wanachama wa TFF ambayo imesajiliwa BMT kama chama cha mchezo wa ridhaa.
Ndiyo, tunaweza kuona baadhi ya klabu zinasajili wachezaji kadhaa kwa kuwalipa mamilioni, mishahara mikubwa, kuwapa posho na kuwapangia nyumba, lakini ukweli utabaki bado hatuna soka la kulipwa.
Soka la kulipwa halihitaji wachezaji wachache tu walipwe vizuri, soka la kulipwa ni biashara kubwa katika kuiwezesha klabu husika kutengeneza biashara na vitega uchumi mbalimbali kwa ajili ya kujiendesha kwa ufanisi kisoka na kiuchumi.
Soka la kulipwa ni biashara, klabu zinatakiwa kuuza hisa ili kupata mitaji ya kuanzisha vitega uchumi, pia klabu zinatakiwa kuuza bidhaa zitakazokuwa na nembo ya klabu kama vile kofia, jezi, fulana na vitu vingine vingi kulingana na ubunifu wa klabu husika.

Klabu inapojiendesha kibishara ina maana inaweza kuchukua mkopo benki kama mtaji wa kuanzisha au kuendeleza miradi yake, lakini kwa mfumo huu wa soka kuendeshwa kiridhaa klabu zetu haziwezi kufanya hivyo.
Ni wazi bado tuna safari ndefu ya kuwa na soka la kulipwa kwani pia ni klabu chache ambazo angalau zinaonekana zinaweza kukidhi kigezo cha kuingia katika soka la kulipwa.
Lakini hata hivyo TFF kuendelea kusajiliwa BMT kama chama cha mchezo wa ridhaa kunafanya safari ya kupata kweli soka la kulipwa kuwa ndefu na ndiyo maana naona hatuna soka la kulipwa.

No comments: