Wednesday 23 July 2014

Simba yasajili Kiungo mpya Toka Kenya

UONGOZI mpya wa Simba hautaki mchezo msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambapo kiungo wa kimataifa wa Kenya, Paul Mungai Kiongera anatarajiwa kutua nchini leo kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kujiunga na klabu hiyo.
Kwa mujibu wa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Usajili ya Simba, mchezaji huyo wa KCB ya Ligi Kuu ya nchini humo, anakuja nchini kwa mazungumzo ya mwisho baada ya mazungumzo ya awali kwa simu na kama yatakwenda vizuri, atasaini Mkataba.
Pia kiungo Mrundi Pierre Kwizera baada ya kufikia makubaliano na uongozi wa Simba anarejea Ivory Coast kumalizana na klabu yake, Afad Abidjan ili aje kusaini mkataba Simba.
Pia klabu hiyo inazidi kujiimarisha zaidi ambao wapo kwenye mazungumzo na klabu za JKT Ruvu, Ruvu Shooting na Coastal Union kwa ajili ya kuwanunua wachezaji Edward Charles, Elias Maguri na Abdul Banda.
Kwa upande mwingine, Simba SC itakutana na wachezaji wake ambao bado wana mikataba, lakini haiwahitaji kwa sasa ili kujadiliana nao kuvunja mikataba yao.
Wachezaji hao ni kipa Abuu Hashimu, beki Hassan Khatib, viungo Abulhalim Humud ‘Gaucho’, Ramadhani Chombo ‘Redondo na washambuliaji Betram Mombeki na Christopher Edward.
Tayari Simba SC imefikia makubaliano ya kuachana na beki Mrundi, Kaze Gilbert anayetakiwa na klabu yake ya zamani, Vital’O.

No comments: