Thursday 24 July 2014

Sumaye awaasa wafuasi wa dini Mbalimbali kuacha kupigana Vita

Mzee Sumaye
 Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesema vita ya kidini na ile inayosababishwa na imani ya watu ni mbaya na mara zote huwa haina mshindi.
Sumaye aliyasema hayo mjini Arusha jana alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa Dayosisi ya Arusha, uliofanyika kwenye Ukumbi wa Sekondari ya Peace House.
“Tanzania hatuna tatizo kubwa katika hili, lakini hatuko salama sana. Kuna chokochoko za hapa na pale zinazoendelea zenye sura ya kiimani. Hii ni ishara ya kuwa upendo, amani na mshikamano miongoni mwetu umepungua na kuathiri umoja wetu.
“Tukiwa wamoja, sekeseke hili halitakuwa na nafasi kwetu kwa sababu hakuna dini inayofundisha chuki wala kupigana, lazima tuwe makini licha ya kila mtu kuwa na uhuru wa kuabudu bila kuvunja sheria,” alisema Sumaye.
Alitoa wito kwa viongozi wa dini kuwasimamia vyema waumini wao ili nchi isije ikakumbwa na balaa la vurugu za kidini, jambo ambalo alisema ni la hatari kwa usalama wa nchi na watu wake.
Alisema wakati dunia inapita katika mapito mbalimbali ya hatari, Watanzania hawana budi kung’ang’ania amani na upendo walionao kwa masilahi ya ustawi wa jamii yao.
Alisema kuna nchi nyingi duniani ambazo zimeingia katika migogoro iliyosababishwa na chuki za kidini na zimeishia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Aliwataka Watanzania katu wasikubali kuruhusu hali hiyo itokee, bali waendeleze misingi ya amani, upande na utulivu vilivyoachwa na waasisi wa taifa, akiwemo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

No comments: