Sunday 20 July 2014

Terry amkabidhi majukumu Cesc Fabregas

BEKI wa Chelsea, John Terry, amesema kazi zote alizokuwa akifanya Frank Lampard kwenye kikosi hicho zimepata mrithi makini na kusisitiza kwamba Cesc Fabregas anaiweza kazi hiyo.
Lampard, 36, ameruhusiwa kuondoka klabuni hapo baada ya mkataba wake kumalizika na kwenda kujiunga na klabu ya Ligi Kuu Marekani, New York City.
Baadaye Chelsea ikamnasa Fabregas kutoka Barcelona na kumsainisha mkataba wa miaka mitano huku akitua Stamford Bridge kwa ada ya Pauni 30 milioni.
Lakini, wakati mashabiki wakiwaza itakuwaje kwa kiungo mpambanaji wao Lampard kuondoka klabuni hapo. Terry, anaamini Fabregas ataweza kuvaa
vyema viatu vilivyoachwa na Mwingereza huyo ambaye ni kinara wa mabao wa nyakati zote klabuni hapo.
“Huu ni usajili makini sana,” alisema Terry alipozungumza na Jarida linalochapishwa na klabu hiyo.
“Ni mzuri sana anapokuwa na mpira. Ni kiungo anayecheza goli hadi goli. Pia amekuwa akifunga mabao kwa wingi na kupiga pasi za maana. Nakumbuka alichokuwa akikifanya alipokuwa Arsenal.
Nina hakika atakuwa mtu muhimu sana klabuni Chelsea kwa sasa na miaka ijayo.” Lampard alitangaza uamuzi wake wa kuihama Chelsea Juni mwaka huu na Terry anakiri wazi kuumizwa na jambo hilo kwa sababu alikuwa swahiba wake wa karibu sambamba na Ashley Cole, aliyetimkia AS Roma.

No comments: